ACT Wazalendo: Wajumbe wa Tume ya Uchaguzi mjiuzulu wenyewe

Mwenyekiti wa ACT Wazalendo na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Masoud Othman (kushoto) akizungumza jambo na aliyekuwa kiongozi wa chama hicho, Zitto Kabwe (kulia) eneo la Nguruka wilayani Uvinza wakati wa mkutano wao na wanachi.

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa Zitto Kabwe, licha ya chama hicho kupigania tume huru na kufanikiwa baada ya sheria kubadilishwa ambayo inataka wajumbe waombe nafasi hiyo, lakini chama cha ACT Wazalendo kinataka wajumbe waliopo waachie nafasi zao na kufanya kama sheria inavyoelekeza.

Mwanza. Chama cha ACT Wazalendo kimesisitiza kwamba wajumbe wa Tume ya Uchaguzi waachie ngazi ili mpya ipatikane kutokana na mchakato wa sheria mpya unaotaka watu waombe, wafanyiwe usaili, majina yapelekwe kwa Rais kwa ajili ya kutangazwa kupata makamishina wapya.

Akizungumza jana Mei 8, 2024 katika kata ya Nguruka wilayani Uvinza, mkoani Kigoma  aliyekuwa kiongozi wa zamani wa chama hicho, Zitto Kabwe amesema licha ya chama hicho kupigania tume huru na kufanikiwa kwa sheria kubadilishwa ambayo inataka wajumbe waombe nafasi hiyo, lakini wanataka wajumbe waliopo waachie nafasi zao na kufanya kama sheria inavyoelekeza.

“Sasa hivi tuna changamoto ya tume ya uchaguzi, tumepigania tume huru ya uchaguzi, tumetunga sheria mpya ya tume ya uchaguzi ambayo haikuwepo, sheria ambayo inataka wajumbe wa tume ya uchaguzi wanatakiwa wapatikane kwa ushindani, watu waombe, washindanishwe, wakishafanyiwa usahili ndio wateuliwe, ndio tume huru ya uchaguzi.

“Tunataka tume ya uchaguzi ambayo wakurugenzi wa halmashauri wasiwe wasimamizi wa uchaguzi, walichofanya Serikali wamewabadilisha jina kutoka kwenye tume ya uchaguzi kuwa tume huru ya uchaguzi. Sisi hatutaki mambo ya kubadilisha majina, tunataka tume kwelikweli ndio maana kauli yetu sisi ni kwamba wajumbe wa tume ya uchaguzi ya sasa waachie ngazi,” amesema Zitto.

Wakiwa njiani kuelekea mkoani Tabora kwa ajili ya ziara ya mwenyekiti wa chama hicho na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman ya kusikiliza changamoto za wananchi, Zitto amesema wataendelea kupigania uwepo wa Katiba mpya ambayo itawapa muungano ambao ni wa haki, usawa, wakuheshimiana.

“Tunaunga mkono muundo wa Muungano wa Serikali tatu, ya Tanganyika, Zanzibar na Muungano lakini hatutaki tupate Serikali ya Tanganyika eti kwa sababu Zanzibar wana Serikali yao, la hasha! Tunataka kupata Serikali ya Tanganyika kwa sababu muundo wa Muungano stahiki ni muundo wa muungano wa Serikali tatu,” amesema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa chama hicho, Masoud Othman amesema ili kuondoa mengi yanayolalamikiwa na wananchi, mageuzi yanahitajika na yanawezekana iwapo wananchi wenyewe wataamua.

“Uchaguzi ukiwa wa haki, mtu mwizi mtamuondoa, wenzetu wanaendelea kwa sababu wanaendesha nchi zao kwa kuwajibishana, kwa uadilifu, katika nchi za wenzetu rushwa ni kosa kubwa sana, hapa kwetu rushwa maana yake mtu akichukua hela lakini kwa wenzetu rushwa ambayo hawakusamehe ni kutumia vibaya madaraka yako ya umma kwa masilahi yako binafsi, kuitumia vibaya ofisi yako.

“Kwa hivyo, ndugu zangu lazima tufike mahala kama tunataka tutoke hapa, kama tunataka tufike safari yetu lazima tubadilishe dereva, Tanzania yetu ni nchi nzuri…tuna tatizo la dereva,” ameongeza.