ACT Wazalendo washauri sakata la mahindi limalizwe kidiplomasia

Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe

Muktasari:

Chama cha ACT Wazalendo kimeitaka Serikali ya Tanzania kukaa mezani na Serikali ya Kenya kumaliza mzozo wa soko la mahindi ya Tanzania yaliyozuiwa nchini humo.

Dar es Salaam. Chama cha ACT Wazalendo kimeitaka Serikali ya Tanzania kukaa mezani na Serikali ya Kenya kumaliza mzozo wa soko la mahindi ya Tanzania yaliyozuiwa nchini humo.

Zuio la mahindi ya Tanzania lilitolewa Machi 5, 2021  na Mamlaka ya Kilimo na Chakula ya Kenya ikidai kuwepo kwa magonjwa ya sumu kuvu katika mahindi yanayotoka Tanzania na Uganda.

Taarifa iliyotolewa leo Jumatatu Machi 8, 2021  na idara ya habari ya ACT Wazalendo inamnukuu Zitto akisema sababu iliyotolewa na Kenya kuwa mahindi ya Tanzania yana sumu kuvu ni kisingizio, bali kuna mambo ya kidiplomasia yanapaswa kusuluhishwa. 

“Hili ni jambo la kidiplomasia sio sumu. Sumu imetumika tu kama sababu. Ni Biashara hii nchi zetu zimekuwa zikifanya juhudi za pamoja kukabiliana na aflatoxin (sumu kuvu) na ushahidi ni sheria pendekezwa za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC),” amesema.

Amesema mahindi ya Tanzania ni salama na ndiyo hayohayo yanayoliwa nchini.

Huku akirejea matatizo ya masoko yaliyoyakumba mazao ya mbaazi na korosho, Zitto ameitaka Serikali kuwalinda wakulima kwa kutumia diplomasia ya uchumi.

“Tunalazimika kuisukuma Serikali ya Tanzania imalize tatizo hili kwa kuzungumza kidiplomasia na Serikali ya Kenya, jambo la kidiplomasia, pande hizo mbili zinapaswa kukaa na kuzungumza ili kusuluhisha mgogoro uliopo.”

“Hiyo amri (ya kuzuia mahindi ya Tanzania kuingia Kenya) haipaswi kuwa juu ya mkataba wa EAC na Itifaki ya soko la pamoja la Afrika Mashariki. Kila mwanachama wa EAC lazima aheshimu mkataba na Itifaki. Aflatoxin imetumika kama sababu tu lakini sio hoja,” amesema.