ACT Wazalendo wataka Serikali iongeze fedha za elimu bila malipo
Msemaji wa Sekta ya Tamisemi na Maendeleo Vijijini wa chama cha ACT Wazalendo, Kulthumu Mchuchuli akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Jumatatu Aprili 17, 2023 wakati akichambua hotuba ya bajeti ya Tamisemi iliyowasilishwa bungeni na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Angela Kairuki.Picha na Michael Matemanga
Muktasari:
- Chama hicho kimebainisha kwamba ufinyu wa bajeti katika kugharamia elimu inayotolewa kwenye shule za msingi na sekondari umekuwa ukiathiri viwango vya ubora wa elimu, hivyo wanaona suluhisho pekee ni kuongeza bajeti ili wanafunzi wapate mahitaji muhimu shuleni kama vile vitabu.
Dar es Salaam. Chama cha ACT Wazalendo kimeitaka Serikali kuongeza kiwango cha ruzuku kwa shule za msingi na sekondari kwa kiwango cha Sh25,000 kwa mwanafunzi wa shule ya msingi na Sh58,000 kwa mwanafunzi wa sekondari ili kuboresha viwango vya ubora wa elimu inayotolewa.
Vilevile, chama hicho kimeitaka Serikali kulipa fidia ya ada na michango mingine ili kuwezesha uendeshaji wa shule kwa kuwa tathmini zinaonyesha ruzuku hiyo haikutokana na tathimini ya gharama halisi za uendeshaji.
Hayo yamebainishwa leo, Aprili 18, 2023 na msemaji wa sekta ya Tamisemi na Maendeleo Vijijini wa ACT Wazalendo, Kulthumu Mchuchuli wakati akichambua hotuba ya bajeti ya Tamisemi iliyowasilishwa bungeni Aprili 14, 2023 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Angela Kairuki.
Mchuchuli amesema viwango vilivyowekwa na Serikali kama ruzuku ambayo ni Sh10,000 kwa mwanafunzi wa shule ya msingi na Sh25,000 kwa mwanafunzi wa sekondari kama ruzuku vimepitwa na wakati kutokana na uhalisia wa maisha na mabadiliko ya thamani ya shilingi dhidi ya dola.
"ACT Wazalendo tunaitaka Serikali kuongeza kiwango cha ruzuku kwa shule za msingi na sekondari kwa kiwango cha Sh25,000 kwa mwanafunzi wa shule ya msingi na Sh58,000 kwa mwanafunzi wa sekondari.
"Pia, Serikali ilipe fidia ya ada na michango mengine ili kuwezesha uendeshaji wa shule kwa kuwa tathmini zinaonyesha ruzuku hii haikutokana na gharama halisi za uendeshaji," amesema Mchuchuli.
Ameongeza kwamba chama chake kinaunga mkono mfumo wa elimu bila malipo ulioanzishwa mwaka 2016, hata hivyo utekelezaji wake umekuwa na changamoto za kibajeti.
Msemaji huyo amebainisha kwamba katika bajeti ya mwaka 2022/2023, Ofisi ya Rais, Tamisemi iliidhinishiwa jumla ya Sh346.49 bilioni kwa ajili kugharamia programu ya elimu msingi na sekondari bila ada, lakini hadi kufikia Februari 2023 Sh235.75 bilioni ndiyo zimepokelewa, sawa na asilimia 68.04.
Amesisitiza kwamba kusuasua kwa kutolewa kwa fedha hizo kunaathiri uendeshaji wa shughuli muhimu za kuboresha elimu. Vilevile, Msemaji huyo ameeleza kwamba ruzuku ya uendeshaji wa shule ni finyu.
"Ni wazi kuwa ufinyu na ucheleweshwaji wa utekelezaji wa bajeti unaathiri kiwango cha elimu na taaluma kwenye shule nyingi kutokana na kukosa uwezo wa kutimiza mahitaji muhimu ya kutoa elimu bora kama vile ukarabati wa miundombinu na ununuzi wa vifaa vya kufundishia na nyenzo za kujifunzia.
"Ndio maana tunaona kuibuka kwa wimbi kubwa la michango inayo elekezwa kwa wazazi kwenye shule mbalimbali nchini. Wazazi wanachangishwa fedha kwa ajili ya mitihani, vitabu, chakula, walinzi, ukamilishaji wa madarasa na kadhalika. Ni dalili za wazi ruzuku na bajeti ya Serikali haijitoshelezi kufikia lengo la kutoa elimu iliyo bora bali ni bora elimu," amesema Mchuchuli.