ACT-Wazalendo yamkalia kooni Mkurugenzi ZEC

Muktasari:

  • Baada ya kufanya mikutano Dar es Salaam, Unguja, ACT-Wazalendo wamehamia Pemba wakisisitiza, bosi wa ZEC aondolewe katika nafasi hiyo huku, pamoja na watendaji na bodi ya wakurugenzi na menejimenti ya bandari ya Malindi ivunjwe.

Dar es Salaam. Chama cha ACT-Wazalendo, kimeendelea kukomaa na sakata la uteuzi wa Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi wa Zanzibar (ZEC), Thabit Idarous Faina, kikisema kitafanya kila liwezekanalo ili mtumishi huyo aachie ngazi.

 Kinacholalamikiwa na ACT -Wazalendo ni kwamba Faina ndiye alikuwa bosi wa ZEC katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 ulioshuhudia wagombea wao zaidi ya 16 wakienguliwa bila sababu za msingi, huku mchakato huo ukifanyika katika mazingira yasiyokuwa huru na wala ya haki.

Mbali na hilo, pia viongozi wa ACT-Wazalendo, wameendelea kukomaa na msimamo wao kuhusu mwenendo usio wa ufanisi wa Bandari ya Zanzibar, wakisema watendaji wa eneo hilo wameshindwa kutelekeza majukumu yao vema na wanapaswa kuondolewa na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi.

Februari 28, mwaka huu Dk Mwinyi alijibu tuhuma hizo za Bandari ya Malindi zilitolewa na Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe katika mkutano wa hadhara uliofanyika Nungwi.

Katika majibu yake, Dk Mwinyi alisema tuhuma hizo si za kweli bali zinalenga kupotosha umma, akisema tatizo la bandari hiyo ni uchache wa gati unaosababisha msongamano wa meli.

Leo Jumamosi Machi 4, 2023, akiwa katika mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa Tibirinzi Pemba, Katibu Mkuu wa Ado Shaibu amewahakikisha Wazanzibari kuwa chama hicho kipo pamoja na wao na watahakikisha bosi huyo wa ZEC anaoondelewa katika nafasi hiyo.

“Haiwezekani mtu aliyesimamia uchaguzi uliokumbwa na changamoto mbalimbali anarudishwa katika nafasi ilele... hatutakubali hata kidogo au nyie mnamtaka Faina? Basi tuseme mara tatu faina aondoke…Faina hatumtaki,” amesema Ado.

Pia, Ado amesema viongozi wa ACT-Wazalendo, hawatakubali uchaguzi wa mwaka 2025 ufanyike kwa kura ya mapema visiwani humo. Alisema watapambana kuhakikisha kura ya mapema inafutwa, haitumiki katika mchakato huo.

Kuhusu mwenendo wa Bandari ya Malindi, Mjumbe wa Kamati Kuu ya ACT-Wazalendo, Ismail Jussa Ladhu alianza kwa kusema yaliyozungumzwa na viongozi wa chama hicho, katika mkutano wa Nungwi, Serikali imewajia juu, akisema hali ni dalili kwamba dawa imeingia taratibu.

“Ukweli ni wameshindwa, wanatafuta kisingizio, katika ukanda wa Afrika kusafirisha kontena na kufika gharama zake ni dola za Marekani 2,000, lakini kufikisha kontena hilo katika bandari ya Zanzibar gharama yake ni dola 7,000.

“Tuliwaambia viongozi wanaojitambua hawanung’nuki na kulia bali wanakuja na majawabu ya changamoto, sasa katika majibu yake (Dk Mwinyi) hakukanusha hata moja, maana yake amethibitisha aliyosasema Zitto.

Jussa amedai kuwa watendaji waliowekwa na Serikali katika eneo hilo, wameshindwa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi, akisema kila mtu analalamikia.

Katika majibu yake, Dk Mwinyi kinachohitaji ni bandari kubwa zaidi itakayokuwa na gati nyingi, ndicho kinachofanywa na Serikali kwa sasa kwa kuwa na mpango wa kujenga bandari ya Mangapwani.

“Kuendelea kulaumu kwa kitu kilichokuwepo kwa miaka yote, mimi sio kama ni sahihi, lakini tumechukua hatua hapohapo Malindi tumeagiza zana mpya, zinazoongeza uharaka wa kushusha mizigo ili kuondoa matatizo, lakini hayataisha kwa muda mfupi,” amesema Dk Mwinyi.