ACT-Wazalendo yasisitiza tume huru kuelekea katiba mpya

Saturday May 07 2022
actpic

Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo, Juma Duni Haji

By Peter Saramba

Mwanza. Chama cha ACT-Wazalendo kimesisitiza msimamo wa kudai marekebisho ya sheria ya vyama vya siasa na uchaguzi kuruhusu kupatikana wa tume huru ya uchaguzi ili kuweka mazingira bora ya kuandikwa kwa Katiba mpya.

Msisitizo huo umetolea leo Jumamosi Mei 7, 2022 jijini Mwanza na Mwenyekiti wa chama hicho, Juma Duni Haji wakati wa kongamano maalum la operesheni "Tume Huru kuelekea Katiba Mpya"

"Kuna mjadala kuhusu nini kianze kati ya tume huru ya uchaguzi na katiba mpya, wapo wanaofananisha jambo hili na hadithi nani wa kwanza kati ya kuku na yai. Sisi ACT-Wazalendo tunasema tuanze na tume huru tukijadiliana masuala ya katiba.

"Sisi ACT-Wazalendo hatupingani na wazo la katiba mpya, lakini tutapataje katiba mpya bila kuwa na tume huru itakayosimamia kura za maoni? Hii tume ya uchaguzi iliyopo haiwezi kazi hiyo kwa sababu haiko huru kuanzia muundo wake na uteuzi wa wajumbe," amesema Makamu Mwenyekiti huyo

Amesema ili kupata tume huru, ACT-Wazalendo inapendekeza wajumbe wake wateuliwe baada ya kupendekezwa na wadau wote kupitia majadiliano na maridhiano ya wote.

"Tukishapa tume huru ya uchaguzi tuanze mchakato wa katiba mpya kuanzia rasimu ya tume ya marekebisho ya katiba ya Jaji Joseph Warioba. Tuachane na ile katiba inayopendekezwa kwa sababu inakinzana na maoni ya wananchi," amependekeza Duni maarufu kama "Babu Duni"

Advertisement

Ameviomba vyama vingine vya upinzani, wanaharakati na wadau wa siasa nchini kuunga mkono hoja ya marekebisho ya sheria kuwezesha kukamilika kwa mchakato wa kupata tume huru itakayosimamia uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 na uchaguzi mkuu wa 2025.

Advertisement