ACT Wazalendo yavuna wanachama kutoka Chadema

ACT Wazalendo yavuna wanachama kutoka Chadema

Muktasari:

  • Uongozi wote wa Chadema Kata ya Dondo, Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani, wamejiondoa kwenye chama hicho na kujiunga na ACT-Wazalendo.

Mkuranga. Uongozi wote wa Chadema Kata ya Dondo, Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani, wamejiondoa kwenye chama hicho na kujiunga na ACT-Wazalendo.


Katika orodha hiyo, yumo aliyekuwa mgombea udiwani wa kata hiyo kupitia Chadema mwaka 2020, Masoud Darwesh ambaye mpaka anajiondoa kwenye chama hicho alikuwa mjumbe wa Kamati ya Chadema ni msingi Kanda ya Pwani.


Mwenyekiti wa Kanda ya Pwani wa Chadema, Baraka Mwago amekiri kuondoka kwa makada hao.


“Ni kweli Daruwesh amekihama chama na tumethibitisha kwa kumuona katika mitandao, ila naomba kuweka sawa si viongozi wote wa Wilaya ya Mkuranga wamehama, tunaye Katibu wetu anaendelea na majukumu yake kama kawaida,” amesema.


Akitangaza uamuzi huo wa kuondoka Chadema mbelea ya waandishi wa habari jana Septemba 19, 2021, aliyekuwa Mwenyekiti wa Kata ya Dondo, Abass Ndambwe amesema wamechukua uamuzi huo baada ya uongozi wa Chadema ngazi za juu kuwatelekeza tangu uchaguzi Mkuu mwaka 2020.


Amesema kwakuwa wao ni wanamageuzi halisi wameamua kuendelea na mapambano ya kudai haki na mapinduzi ya kweli ya fikra kupitia ACT Wazalendo.


Ndambwe amesema tangu kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu mwaka jana 2020 wagombea wa vyama vingine  hawajawahi kuwatembelea isipokuwa ACT Wazalendo kupitia kwa aliyekuwa mgombea wake wa Ubunge wa Jimbo la Mkuranga, Mohamed Mtambo ambaye amekuwa nao bega kwa bega  wakati wote.
Amesema licha ya Mtambo kutokufanikiwa kushinda ubunge, hajakata tamaa bali ameendelea kuwajulia hali na kubadilishana nao mawazo kwa kila hali.


"Sisi lengo letu ni lile lile la kuunganisha umma kujua haki zao kupitia mageuzi ya kifikra na hatimaye kuiondoa CCM madarakani, tunaamini kupitia ACT Wazalendo malengo hayo yatatimia.


Naye aliyekuwa mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Bawacha Tawi la Mpafu, Zabibu Mlawa amesema wanawake wanaounga mkono vyama vya upinzani wamekuwa wakibaguliwa na Serikali za vijiji hususani katika kupata mikopo kupitia ya kujikwamua kimaendeleo.

Kwa upande wake, aliyekuwa mgombea Ubunge kwa tiketi ya ACT Wazalendo, Mohamed Mtambo aliwapongeza wanachama hao kwa uamuzi huo wa kuendeleza mapambano ya kisiasa kupitia vyama vya upinzani.


"Wananchi hawa wa Kata ya Dondo walinipigia kura nyingi, nami nimeona ni jambo jema kuja kuwashukuru na kujua changamoto zao ili tutafute namna nzuri ya kuzitatua,” amesema Mtambo.