Ada ya mtihani yawagawa wadau

Muktasari:

Mjadala bado unarindima kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vya habari kuhusu uamuzi wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) kufuta ada ya mtihani kwa wanafunzi wa shule za umma.

Mjadala bado unarindima kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vya habari kuhusu uamuzi wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) kufuta ada ya mtihani kwa wanafunzi wa shule za umma.

Uamuzi huo umepokelewa kwa hisia tofauti za kuukubali na hata kuunyooshea kidole, kama anavyosema mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Dk Faraja Kristomus, anayeamini kuwa uamuzi huo utaleta malalamiko na matabaka kwenye mfumo wa elimu nchini, kwa kile anachoeleza kuwa hata wanaosoma shule binafsi nao pia ni Watanzania.

“Kuwabagua kunaweza kuleta matabaka kwa namna moja au nyingine, kusoma shule binafsi haimaanishi kuwa sio Watanzania na wakifanikiwa kielimu, watakuja kuwahudumia Watanzania wote bila ya kujali walisoma wapi, hivyo suala hili lingepaswa kuangaliwa vyema kabla ya uamuzi wa aina hii kufanyika,’ anasema.

Pamoja hilo Dk Kristomus anasema wasiwasi wake pia upo kwenye namna ambavyo Baraza litaweza kujiendesha bila utegemezi wa ada hizo, ambazo zilikuwa zikitumika katika uandaaji na uratibu wa mitihani hapa nchini.

“Baraza la Mitihani litatetereka katika bajeti ya kuendesha shughuli zake za usimamizi wa mitihani. Wanaochangia wengi wanatoka shule za Serikali, kuwafutia ada za mtihani kutasababisha nakisi kubwa ya bajeti kwa Necta. Sina uhakika kama Serikali itafidia hilo pengo na kama imejiandaa kufidia hilo pengo kwa nini isifute kwa shule zote zikiwemo za binafsi? anahoji.

Hata hivyo, anasema njia bora zaidi ingekuwa siyo kufuta ada kabisa bali shule zingepewa jukumu la kubaini watoto wanaotoka katika familia maskini kabisa, na hao ndio waliotakiwa kusamehewa na Serikali.

Naye mdau wa elimu Zaida Mgala anasema kilichofanyika ni hatua kubwa katika kuhakikisha watoto wote wa Tanzania wanapata elimu bila kuwepo kikwazo, lakini akasisitiza kuwa msamaha huo wa ada ya mtihani unapaswa kuwagusa wanafunzi wote bila kujali shule wanazosoma.

“Watoto wa walipa kodi wa Tanzania sio wote wanasoma shule za Serikali, wengine wanasoma shule za binafsi na wengine wanasaidiwa sio kwamba wazazi wao ndio wanawalipia huko, hivyo suala hili nalo lilipaswa kuangaliwa,’’ anaeleza.

Anaongeza: “Kwa maoni yangu naona hii ada ingeondolewa kwa wanafunzi wote bila kubagua maana hata huyo anayesoma shule binafsi , akienda chuo kikuu atakutana na wa shule ya Serikali na mwisho hawa wote watatumia utaalamu wao kuwasaidia Watanzania. Hata hawa wazazi wenye watoto wanaosoma shule za binafsi, wanahitaji kupunguziwa mzigo,” anasema Zaida.

Mhadhiri wa Chuo cha St John, Dk Shadidu Ndossa anasema kufutwa kwa ada ni hatua nzuri na kubwa katika jitihada za kuwapatia ukombozi wa kielimu watoto wa Kitanzania hasa wanaotoka katika familia duni.

“Tunafahamu kuna baadhi ya wazazi hawana uwezo kabisa wa kulipa hii ada hivyo mtoto anaweza kufanya mtihani na matokeo yake yakafungiwa, hivyo naona ni hatua nzuri inayopasa kupongezwa. Yanapozungumziwa maendeleo endelevu kuna lengo linalosisitiza watoto wote wapate elimu msingi na ndicho kinachofanyika.

“Tuchukulie kwamba uamuzi huu kwa siku za usoni utakwenda hadi kwa wanafunzi wa shule binafsi kwa kuwa wote ni Watanzania, na hata elimu yao wataitumia katika maeneo mbalimbali hapa nchini, hivyo wana haki ya kunufaika na mpango huu,”anasema Dk Ndossa

Mawazo ya Dk Ndossa hayapishani na ya Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) Anna Henga, anayesema kilichofanyika ni mwendelezo wa mpango wa Serikali katika kuhakikisha watoto wa Kitanzania wanapata elimu bila kujali changamoto za hali ya uchumi zinazozikabili familia nyingi nchini.

‘‘Ukweli ni kwamba hali ya maisha ya Watanzania wengi si nzuri , unaweza kuona fedha hiyo ni ndogo lakini wapo wanaoshindwa na kujikuta ndoto zao zimekatishwa. Niipongeze Serikali kwa hatua hii.. ni uamuzi mzuri wenye lengo la dhati la kuhakikisha watoto kutoka familia maskini wanapata elimu bila kikwazo,”

Kuhusu matabaka, anasema haiwezi kuwa changamoto, kwa sababu wanafunzi wanaosoma shule za kulipia wamekuwa wakilipa fedha nyingi kwenye ada hivyo hata ikiondolewa ada ya mtihani haiwezi kubadilisha kitu.