Adaiwa kumuua mume wa ‘mchepuko’ ili wawe huru

Washtakiwa wanne ambao wote kwa pamoja  wanashtakiwa kwa kosa moja la mauji wakiwa kwenye chumba cha Mahakama Kuu Kanda ya Geita. Picha na Rehema Matowo

Muktasari:

  • Wapenzi hao wanadaiwa kumuua kwa maksudi Tegemeo Rashid kinyume na kifungu cha 196 na 197 cha Sheria ya Kanuni ya adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022, katika Kijiji cha Ihaga, wilayani Chato, mkoani Geita.

Geita. Upande wa Jamhuri, katika kesi ya mauaji ya Tegemeo Rashid, umebainisha sababu za mauaji hayo kuwa ni ugomvi uliotokana na wivu wa kimapenzi, aliokuwa nao mshtakiwa wa kwanza katika kesi hiyo, Elisha Fredrick (31), kwa mke wa marehemu aliyekuwa hawara yake.

Hayo yamebainishwa mahakamani na mwendesha mashtaka katika kesi hiyo, Wakili wa Serikali, Verena Mathias, leo Ijumaa, Aprili 19, 2024, wakati wa usikilizwaji wa awali wa kesi hiyo.

Kwenye hatua hiyo, washtakiwa wamesomewa maelezo ya awali ya kesi, kuhusu namna walivyotekeleza mauaji hayo.

Mbali na Elisha, washtakiwa wengine katika kesi hiyo inayosikilizwa na Jaji Graffin Mwakapeje wa Mahakama Kuu Kanda ya Geita, ni Ndaishega Emmanuel (39), Ezekiel John (42) na Amos Fredrick.

Wote kwa pamoja wanadaiwa kumuua kwa maksudi Tegemeo Rashid kinyume na kifungu cha 196 na 197 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022, wakidaiwa kutenda kosa hilo Novemba 2, 2022 katika Kijiji cha Ihaga, Wilaya ya Chato, mkoani Geita.

Akiwasomea washtakiwa maelezo hayo ya awali, Wakili Mathias ameieleza Mahakama kuwa Novemba 11, 2022 huko katika Kijiji cha Ihaga wilayani Chato saa 12 jioni, Tegemeo alivamiwa na kundi la watu.

Watu hao, amesema walimkata Tegemeo kwa kitu chenye ncha kali sehemu mbalimbali za mwili wake kisha kumfunga kamba na kwamba wavamizi hao pia walikuwa na bunduki waliyoitumia kuwatisha wananchi waliokuwa wanasogea karibu na tukio.

Wakili Mathias amedai kuwa baada ya tukio hilo, taarifa zilimfikia mke wa Tegemeo aitwaye Jesca Josephat ambaye alitoa taarifa kituo cha polisi.

Amefafanua kuwa Jesca aliwaeleza askari polisi kuwa anayehusika na mauji hayo ni Elisha Fredrick (mshtakiwa wa kwanza) kwa kuwa wana uhusiano wa kimapenzi na kwamba mshtakiwa huyo hakuwa tayari kuona ndoa yao ikiendelea.

Kwa mujibu wa maelezo hayo, mwili wa marehemu ulipelekwa katika zahanati ya Bwanga wilayani Chato kwa ajili ya uchunguzi na baada ya uchunguzi huo, chanzo cha kifo kilitajwa kuwa ni maumivu makali kwenye ubongo pamoja na kuvuja damu nyingi.

Wakili Mathias ameeleza kuwa Novemba 3, 2022, mshtakiwa wa kwanza alikamatwa na katika mahojiano na polisi, alikiri kumuua Tegemeo.

Amedai kuwa Novemba 4, 2022 washtakiwa wengine watatu walikamatwa katika mazingira tofauti, akibainisha kuwa mshtakiwa wa pili (Ndaishega) alipopekuliwa alikutwa na kisu na vitu mbalimbali vya marehemu.

Amevitaja vitu hivyo kuwa ni pamoja na kadi ya Benki ya CRDB ya marehemu Tegemeo, risiti za kutoa fedha zenye jina la marehemu Tegemeo na simu aina ya Infinix.

Wakili Mathias amedai kuwa mshtakiwa huyo wa pili alipofikishwa Kituo cha Polisi Buseresere na kuhojiwa kuhusu mauaji hayo, alikiri kuhusika.

Amedai kuwa siku hiyo hiyo, Novemba 4, 2022, mshtakiwa wa nne alikamatwa na alipopekuliwa alikutwa na tiketi zenye majina ya Amos Fredrick na Ezeckiel John.

Amedai kuwa mshtakiwa wa nne alisaidia kupatikana kwa bunduki yenye risasi 11 na alipofikishwa Kituo cha Polisi Buseresere, alihojiwa kuhus mauaji hayo, pia alikiri kutenda kosa hilo.

Wakili Mathias ameongeza kuwa Novemba 8, 2022 katika Kituo cha Polisi Lugambagwe kulifanyika gwaride la utambuzi kwa ajili ya kumtambua mshtakiwa wa pili, wa tatu na wa nne, ambao wote walitambuliwa na mashahidi.

Vilevile, Wakili Mathias ameeleza kuwa washtakiwa wote walichukuliwa alama za vidole ambazo pamoja na vielelezo vingine vilipelekwa kwa wataalamu kwa uchunguzi wa kisayansi.

Kabla ya kusomewa maelezo hayo ya kesi, washtakiwa hao wamesomewa tena shtaka linalowakabili, nao kwa mara ya kwanza wamekana kuhusika nalo.

Baada ya kusomewa maelezo ya kesi, wametakiwa kubainisha mambo wanayoyakubali na yale wanayokataa na washtakiwa wote wamekubaliana na majina yao na taarifa nyingine zinazohusiana na utambulisho wao, lakini wakakana maelezo yote kuhusiana na shtaka linalowakabili.

Mambo hayo waliyoyakana ndio hoja zinazobishaniwa ambazo upande wa mashtaka unapaswa kuwaita mashahidi kuzithibitisha.

Baada ya kukamilika kwa hatua hiyo, Jaji Mwakapeje ameahirisha kesi hiyo hadi kikao kingine cha Mahakama kitakachopangwa na Msajili.

Wakati wa usikilizwaji kamili wa kesi hiyo, upande wa mashtaka utakuwa na mashahidi 29 na vielelezo 13.

Washtakiwa hao wanatetewa na mawakili Constantine Ramadhan, anayemtetea mshtakiwa wa kwanza, Erick Lutehanga anayemtetea mshtakiwa wa pili na watatu na Elizabeth Msechu, anayemtetea mshtakiwa wa tano.