Adaiwa kutumia jina la Angela Mabula kutapeli Sh5.4 milioni
Muktasari:
- Frank Rugeimkamu amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkuu Kisutu kwa kujifanya kuwa aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi, Angeline Mabula na kutapeli Sh5.4 milioni kutoka kwa watu tofauti.
Dar es Salaam. Frank Rugeimkamu amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkuu Kisutu akikabiliwa na mashtaka saba yakiwemo ya kujifanya aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi, Angeline Mabula ili kujipatia Sh5.4 milioni kwa njia ya udanganyifu.
Akisoma mashtaka hayo leo Oktoba 4 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Ushindi Swalo, Wakili wa Serikali Asiath Mzamiru amedai kuwa mshtakiwa huyo anakabiliwa kujifanya mtu mwingine, kujipatia fedha Kwa njia ya udanganyifu na kutumia laini ya simu ya mtu mwingine.
Mzamiru amedai katika shtaka la kwanza tarehe tofauti ndani ya Septemba 2021, mshtakiwa huyo alijifanya kuwa yeye ni aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Angeline Mabula kwa Furaha Dominick huku akijua kuwa si kweli.
Katika shtaka la pili inadaiwa kuwa Mei 22, 2022 katika eneo la Buswelu, wilaya ya Ilemela Mkoa wa Mwanza mshtakiwa huyo alijifanya kuwa Angeline Mabula kwa kutumia ujumbe mfupi kupitia mtandao wa kijamii wa WhatsApp kwa Tabia Mwita, huku akijua si kweli.
Shtaka lingine inadaiwa kuwa tarehe isiyojulikana Mei, 2022 eneo la Buswelu Mkoani Mwanza, mshtakiwa huyo alijifanya kuwa yeye ni Angeline Mabula kwa Zainab Shomari kupitia ujumbe mfupi wa mtandao wa kijamii wa whatsapp huku akijua ni uongo.
Katika mashtaka ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu inadaiwa kuwa Mei 15, 2022 katika eneo la Buswelu wilaya ya Ilemela, Mkoa wa Mwanza mshtakiwa alijipatia Sh1 milioni kutoka kwa Fauz Abdulrazak akidai kuwa zinahitajika na Angeline Mabula.
Mzamiru alidai kuwa katika eneo hilo hilo kati ya Mei 7, 2022 na Juni 22, 2022 mshtakiwa huyo alijipatia fedha kiasi cha Sh 3.5 milioni kutoka kwa Zainab Hamis akidai kuwa fedha hizo zilihitajika na Angeline Mabula.
Pia akiwa eneo la Makao Mapya, Buswelu Mkoani Mwanza katika tarehe isiyojulikana Julai, 2022 inadaiwa kuwa mshtakiwa huyo alijipatia fedha kiasi cha Sh 900,000 kutoka kwa Majid Suleiman akidai kuwa zinahitajika na Angeline Mabula.
Pia mshtakiwa huyo anakabiliwa na shtaka la kutumia laini iliyosajiliwa kwa jina la mtu mwingine ambapo inadaiwa kuwa Septemba 27, 2022 katika eneo la Kyaka mkoani Kagera alikutwa na laini iliyosajiliwa kwa jina la Geoffrey John Gabriely.
Baada ya maelezo hayo Hakimu Swallo alisema kuwa dhamana ya mshtakiwa huyo ipo wazi anatakiwa kuwa na wadhamini wawili wanaotambulika kisheria watakaosaini bondi ya Sh 4.5 milioni.
Hata hivyo mshtakiwa huyo alishindwa kutimiza masharti ya dhamana hiyo hivyo amerudishwa rumande.
Shauri hilo limeahirishwa hadi Oktoba17, 2023 Kwa ajili ya hoja za awali