Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mradi wa KKK Msalato Satelite City

Muktasari:

  • Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Angeline Mabula, amesema mradi wa Kupanga na Kupima na Kumilikisha Ardhi (KKK), eneo la Kitelela mkoani Dodoma, maarufu kama ‘Msalato Satelite City,’ utakuwa wa mfano kwa matumizi mbalimbali.

Dodoma. Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Angeline Mabula, amesema mradi wa Kupanga na Kupima na Kumilikisha Ardhi (KKK), eneo la Kitelela mkoani Dodoma, maarufu kama ‘Msalato Satelite City,’ utakuwa wa mfano kwa matumizi mbalimbali.

Imeelezwa kuwa, Wizara ya Ardhi inatekeleza mradi huo kwa kutwaa eneo katika mtaa wa Kitelela jijini Dodoma, lenye ukubwa wa takriban ekari 971; kisha kulipa fidia, kupanga na kupima eneo kwa ajili ya matumizi mbalimbali ambapo jumla ya viwanja 1,012 vimepimwa.

Akizungumza wakati wa uwasilisha taarifa ya wizara hiyo kuhusu mradi wa KKK, kwa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii, leo Ijumaa Agosti 24, 2023; jijini Dodoma, Dk Mabula amesema, mradi huo utahakikisha huduma mbalimbali zinapatikana katika eneo hilo sambamba na kuzuia ujenzi holela.

Kwa mujibu wa Dk Mabula, Wizara ya Ardhi kwa kushirikiana na Halmashauri ya Jiji la Dodoma katika utekelezaji ‘Mpango Kabambe’ wa jiji hilo, imekuwa ikitekeleza miradi mbalimbali katika Jiji la Dodoma.

‘’Suala la Kitelela, tunataka mradi huu uwe wa mfano, tunataka mradi usimamiwe na uwe tofauti na miradi mingine,’’ amesema Dk Mabula.

Amebainisha kuwa, utekelezaji wa ‘Mpango Kabambe wa Jiji la Dodoma’ unaendana na malengo yaliyoainishwa kwenye ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), ya kupanga na kupima viwanja vipatavyo 2,500,000 kwa miaka mitano (2020-2025).

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wizara hiyo, Mhandisi Anthony Sanga, amesema kupitia mradi huo wa Kitelela, fedha zitakazopatikana zinatarajiwa kutumika kwa ajili kuanzisha miradi mipya kwenye maeneo mbalimbali nchini.

‘’Mradi wa Kitelela tunaufanya kama ‘demo’ na fedha zinazopatikana kupitia mradi huo zitumike kutwaa na kupima maeneo mengine, hii ni moja ya mikakati ambayo wizara inaendelea nayo,’’ amesema Mhandisi Sanga.

Awali wajumbe wa hiyo wameipongeza wizara kwa kubuni na kutekeleza mradi wa KKK. Hata hivyo, wameitaka wizara hiyo kuhakikisha inadhibiti mapema ujenzi holela na kuacha kusubiri kufanya zoezi la urasimishaji makazi.

‘’Naipongeza Wizara kwa namna ilivyojipanga lakini ni vizuri ikawa pro- active hasa kwa ile miji inayokuwa na kuacha kusubiri kurasmisha makazi,‘’ amesema Shaban Shekilindi, mjumbe katika kamati hiyo na Mbunge wa Lushoto, mkoani Tanga.

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Geofrey Pinda kwa upande wake amesema, wizara hiyo kwa sasa iko kazini na kwamba wajumbe wa kamati hiyo wanapaswa kuimani katika masuala mbalimbali inayotekeleza.

‘’Wizara iko kazini naomba mtuamini ili tuweze kutekeleza majukumu yetu na mwisho wa siku hii migogoro ya ardhi iweze kupungua kama siyo kuisha’’ alisema Pinda.

Kwa upande mwingine, wizara hiyo imewasilisha taarifa zake mbili za utekelezaji mapendekezo ya Kamati maalum ya mawaziri nane wa kisekta, juu ya utatuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji 975, pamoja na utekelezaji wa program hiyo ya KKK.