Adakwa akidaiwa kusafirisha bangi

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Muktasari:

  • Polisi mkoani Mbeya inamshikilia kijana mmoja kwa tuhuma za kukamatwa na kilo 13 za bangi, akiwa njiani kuelekea stendi ya mabasi Kyela kwa lengo la kuusafirisha kwenda jijini Dar es Salaam.

Mbeya. Jeshi la Polisi mkoani Mbeya, linamshikilia Kelvin Amanyisye (19) mkazi wa Lubele katika mpaka wa Kasumulu, Wilaya ya Kyela, kwa tuhuma za kupatikana na dawa za kulevya aina ya bangi kilo 13.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga ameyasema hayo leo Jumamosi Desemba 30, 2023 wakati wa mkutano na wanahabari, huku akisema mtuhumiwa alikamatwa katika kivuko kisicho rasmi cha eneo la boda ya zamani.

Kuzaga amesema kuwa mtuhumiwa baada ya kupekuliwa alikutwa akiwa na dawa hizo kwenye mifuko ya ‘Rambo’ 13, kisha kufichwa kwenye begi kubwa alilolipakiza kwenye pikipiki.

“Mtuhumiwa alikuwa akielekea stendi ya mabasi Kyela kwa ajili ya kusafirisha mzigo huo kuelekea jijini Dar es Salaam ambapo kwa sasa anahojiwa, atafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika,” amesema Kuzaga.

Sambamba na hilo Kamanda Kuzaga amesema katika kuelekea sikukuu ya mwaka mpya 2024, jeshi hilo limejipanga vizuri kuimarisha ulinzi na usalama wa raia na mali zao mkoani hapa.

Wakati huo huo ametoa onyo kali ama kwa mtu au watu ambao hawana kibali cha kupiga fataki, kujihusisha na mchezo huo kwa kuwa mpaka sasa jeshi hilo limetoa kibali kimoja tu.

Aidha, Kamanda Kuzaga amepiga marufuku wananchi kujishusha kuchoma moto matairi katika barabara na kusababisha uharibifu, “Watakaobaini kufanya watachukuliwa hatua kali za kisheria.