Adhana yamsimamisha Kenyatta kusoma hotuba Dodoma

Muktasari:
- Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta amesimamisha hotuba yake kwa zaidi ya dakika moja kupisha wito wa swala (adhana) ya adhuhuri wakati akitoa salamu za pole kwa Watanzania katika shughuli ya kumuaga aliyekuwa Rais wa Tanzania, John Magufuli.
Dodoma. Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta amesimamisha hotuba yake kwa zaidi ya dakika moja kupisha wito wa swala (adhana) ya adhuhuri wakati akitoa salamu za pole kwa Watanzania katika shughuli ya kumuaga aliyekuwa Rais wa Tanzania, John Magufuli.
Wakati akianza kutoa salamu zake katika uwanja wa Uhuru jijini Dodoma adhana ilisikika kutoka katika msikiti uliopo karibu na uwanja huo na kumfanya kiongozi huyo kusitisha kwa muda kutoa hotuba yake na adhana ilipomalizika aliendelea na maelfu ya watu waliopo uwanjani hapo walimpigia makofi.
Katika hotuba yake Kenyatta amemwomba Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kuendeleza falsafa ya Hapa Kazi Tu aliyoiacha Magufuli kwa kuwa inawafanya Watanzania kuwa na moyo wa ushujaa na kusonga mbele.
Amemtaka Rais Samia kujipa moyo wa ushujaa bila kuteteleka na kuwa Kenya itakuwa pamoja naye wakati wote.
"Katika maandiko ya Biblia Mungu alimwambia Joshua kuwa ‘uwe hodari na moyo wa ushujaa na usiogope kokote uendako Mungu yu pamoja nawe’," amesema Uhuru.
Amesema enzi za uhai wa Magufuli walizungumza kuhusu maendeleo na usalama wa nchi hizo mbili.
Rais Kenyatta amezungumzia maamuzi aliyokuwa akiyafanya Magufuli kuhusu miradi mikubwa aliyoifanya nchini mwake badala ya kutegemea watu wa nje.