Afutiwa kesi ya mirungi, akamatwa tena na kupelekwa DCEA

Mshtakiwa Rhoda Salum, akiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya kufutiwa kesi yake na kisha kukamatwa tena na kupelekwa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya( DCEA).

Muktasari:

  • Mshtakiwa anadaiwa kutenda kosa hilo, Januari 26, 2023 eneo la Wailes wilaya ya Temeke, ambapo anadaiwa kukutwa na kilo 23.84 za mirungi, kinyume cha sheria.

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemfutia kesi mshtakiwa, Rhoda Salum (48), aliyekuwa anakabiliwa na shtaka la kusafirisha kilo 23.84 za dawa ya kulevya aina ya mirungu, baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) kuieleza Mahakama hana nia ya kuendelea na shauri hilo dhidi ya mshtakiwa huyo.

Mshtakiwa alikuwa anakabiliwa na shtaka moja la kusafirisha dawa hizo, tukio analodaiwa kulitenda Januari 26, 2023 katika mtaa wa Wailes uliopo Wilaya ya Temeke

Kesi hiyo ilikuwa katika hatua ya usikilizwaji na tayari mashahidi sita wa upande wa mashtaka walikuwa wametoa ushahidi wao dhidi ya mshtakiwa.

Hadi inafutiwa kesi hiyo, leo Jumatatu, April 15, 2024, Rhoda amekaa garezani siku 424, ambazo ni sawa na mwaka mmoja, mwezi mmoja na siku 28 kutokana na shtaka linalomkabili halina dhamana kwa mujibu wa sheria.

Kwa mara ya kwanza, Rhoda alifikishwa mahakamani hapo Februari 16, 2023  kujibu shtaka linalomkabili.

Rhoda amefutiwa kesi yake na hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Richard Kabate, baada ya Wakili wa Serikali Eva Kassa, kuwasilisha hati ya kutokuwa na nia ya mashtaka dhidi ya mshtakiwa huyo.

Mshtakiwa huyo amefutiwa shtaka lake chini ya kifungu namba 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), sura ya 20, iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022.

Akimfutia kesi hiyo, Hakimu Kabate amesema kutokana na hati hiyo iliyowasilisha chini ya kifungu hicho, Mahakama inamwachia mshtakiwa kwa sababu upande wa mashtaka hawana nia ya kuendelea na kesi dhidi washtakia.

Hata hivyo, muda mfupi baada ya kufutiwa kesi, Rhoda amekamatwa na askari Polisi waliokuwepo mahakamani hapo kuwekwa chini ya ulinzi, kisha kupelekwa ofisi za Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA).


Kabla ya kufutiwa kesi:

Kabla ya kufutia kesi hiyo, Wakili Kassa ameieleza Mahakama hiyo kuwa kesi hiyo ililetwa kwa ajili ya kuendelea na ushahihidi wa upande wa mashtaka, lakini DPP hana nia ya kuendelea na shauri hilo mahakamani hapo.

 Mshtakiwa alimuandikia barua DPP

April 2023, Rhoda, alimuandikia barua (DPP), akiomba kukiri shtaka lake na kupunguziwa adhabu, ili amalize kesi hiyo.

Baada ya kuandika barua hiyo, Serikali ilianza vikao vya majadiliano ya kuimaliza kesi hiyo dhidi ya mshtakiwa huyo.

Hata hivyo, majadiliano ya kukiri shtaka hilo, kati ya Rhoda na DPP, yalikwama na ndipo Februari 29, 2024 Serikali ilipoamua kumsomea hoja za awali (PH) mshtakiwa huyo na kisha kuanza kusikiliza ushahidi.


Hati ya mashtaka

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, Rhoda anadaiwa kutenda kosa hilo, Januari 26, 2023 eneo la Wailes, lililopo wilaya ya Temeke.

Inadaiwa siku hiyo ya tukio, mshtakiwa huyo alikutwa akisafirisha kilo 23.84 za Mirungi, kinyume cha sheria.