Ahadi tatu za Bashiru kwa Magufuli

#Live: Kuapishwa kwa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dk Bashiru Ally

Muktasari:

  • Dk Bashiru aliyeapishwa leo Ikulu ya Dar es Salaam ameahidi kufuata nyayo za mtangulizi wake, Dk John Kijazi kutekeleza majukumu ya wadhifa wake mpya.

Dar es Salaam. Katibu mkuu kiongozi, Balozi Bashiru Ally ameapishwa kushika wadhifa huo leo Jumamosi Februari 27, 2021 Ikulu Dar es Salaam na kuahidi mambo matatu ikiwemo kuimarisha mawasiliano kati ya Serikali na wananchi.

Dk Bashiru ambaye pia ni katibu mkuu wa CCM, aliteuliwa na Rais John Magufuli jana Ijumaa Februari 26, 2021 kuwa balozi na katibu mkuu kiongozi kuchukua nafasi ya aliyekuwa katibu mkuu kiongozi, Balozi John Kijazi aliyefariki dunia Februari 17, 2021.

 “Hii ni mara ya pili kunipa fursa maalum, kwanza ndani ya chama chetu na sasa hivi ndani ya Serikali. Imani hiyo nitailipa kwa imani, nikuombee kwa mwenyezi Mungu akupe nguvu, hekima na busara iendelee kutuongoza kwa ujasiri kama unavyofanya,” amesema Dk Bashiru akimwambia  Rais Magufuli.

Amesema atatekeleza maelekezo ya Rais Magufuli ikiwa pamoja na umuhimu wa mawasiliano Serikalini na kati ya Serikali na umma.

“Hili nitalisimamia ili kuhakikisha kwamba Serikali inafanya kama timu moja kupitia  watumishi wa umma, idara, wizara inatoa taarifa kwa haraka kwa wananchi,” amesema.

Pia amesisitiza kuendeleza uzalendo, uadilifu na utumishi kwa wananchi hasa katika kutatua kero zao.

Jambo la tatu alizosisitiza ni umuhimu wa kusimamia haki na kusisitiza wajibu wakila mmoja.

“Umezungumza umuhimu wa vyombo vinavyohusika kuhakikisha kwamba kila uamuzi tunaofanya unazingatia haki hususani haki za wanyonge.”

“Kama ni suala ushuru kodi au tozo mbalimbali, utaratibu wa kisheria unazingatiwa lakini pia kusimamia uwajibikaji ili nchi yetu ipige hatua za kutosha,” amesema.

Akizungumzia uteuzi huo, Dk Bashiru amesema hakuutegemea kwani tayari Rais alikuwa amempa majukumu mengine ya CCM na alikuwa akijiandaa kuyatekeleza.

“Jana jioni nipo nasoma mafaili yangu napata taarifa kuwa umeniteua. Mshtuko huo haunipi kusema mengi. Bado natafakari sana.

“Nitafanya nini nitafanya vipi kukidhi matarajio yako kwa imani uliyonipa kwa mfululizo. Niwaombe Watanzania wote mniombee niweze kukidhi matarajio ya Rais,” amesema.

Huku akiwashukuru viongozi wa CCM, amewaomba viongozi wa Serikali wakiwemo makamu wa Rais,  Samia Suluhu Hassan na waziri mkuu, Kassim Majaliwa pamoja na Bunge na Mahakama kumpa ushirikiano.

Hafla hiyo pia imehudhuriwa na naibu spika, Dk Tulia Ackson, Jaji Mkuu Profesa Ibrahim  Juma, viongozi wa majeshi ya ulinzi na usalama na baadhi ya mawaziri.