Air France -KLM yapata bosi mpya Tanzania

Dar es Salaam. Shirika la ndege la Air France -KLM limemteua Rajat Kumar kuwa Meneja mkazi wa nchini Tanzania, akichukua nafasi ya Alexander van de Wint ambaye alikuwa akihudumu katika nafasi hiyo kwa miaka 6.

Taarifa ya Air France - KLM inamtaja Rajat kama mfanyakazi wao mwenye uzoefu katika huduma za usafiri wa anga wa muda mrefu akishika nyadhifa tofauti ndani ya shirika hilo.

Kabla ya kuteuliwa nchini Tanzania, aliwahi kuwa meneja wa nchi za Kuwait, Qatar na Iran, ambapo alionyesha uongozi wa kipekee na ujuzi wa kimkakati katika kukuza ukuaji wa biashara na huduma kwa wateja.

Miongoni mwa mambo anayokumbukwa nayo ni kusimamia shughuli za shirika hilo wakati wa fainali za Kombe la Dunia la FIFA mwaka 2022, zilizofanyika nchini Qatar na kwa Tanzania, atakuwa na jukumu la kuendesha malengo ya biashara, kuimarisha mahusiano na wateja na kuimarisha nafasi ya shirika hilo katika Soko la Tanzania.

 "Tunafurahi kumkaribisha Rajat kama Meneja mpya wa Air France Tanzania, uzoefu wake wa kina na uongozi wa kimkakati utasaidia katika kusukuma mbele biashara yetu na kutoa thamani ya kipekee kwa wateja wetu nchini Tanzania," alisema Marius van der Ham, Meneja Mkuu wa Air France - KLM Kanda ya Afrika Mashariki na Kusini.

 Rajat alielezea shauku yake kwa majukumu mapya akisema, "Nina furaha kuongoza shughuli za Air France - KLM nchini Tanzania, na ninatarajia kufanya kazi kwa karibu na wadau wote muhimu ili kuimarisha zaidi uwepo wetu sokoni na kutoa usafiri usio na kifani, uzoefu wa chapa zetu kwa wateja wetu."

 Uteuzi wa Rajat unakuja ikiwa ni miezi sita tangu Air France ilipoanza safari za moja kwa moja kutoka Paris-Charles de Gaulle hadi Dar es Salaam na kupanua wigo wake katika ukanda huo kufuatia umaarufu wa njia za Zanzibar na Nairobi.