Ajali ya basi yaua 9 Katavi

Eneo la ajali Mlima Kondwe wilaya ya Tanganyika

Muktasari:

  • Ajali hiyo imetokea Machi 6 saa 9:45 alasiri baada ya basi hilo kuacha njia na kuserereka kwenye korongo hilo lenye kina cha mita zisizopungua 75.

Katavi. Watu tisa wamepoteza maisha na wengine 30 kujeruhiwa baada ya basi la kampuni ya Kombas kuacha njia na kupinduka kwenye korongo la mlima Nkondwe wilayani Tanganyika.

Baadhi ya majeruhi wakiwa hospitali ya wilaya ya Tanganyika

Ajali hiyo imetokea jana Machi 6 saa 9:45 alasiri ambapo imeelezwa kuwa baada ya kufika eneo la mlima Nkondwe basi hilo liliserereka hadi kwenye korongo hilo lenye kina cha mita zisizopungua 75 chini yake kukiwa na mto.

Mganga Mkuu hospitali ya wilaya ya Tanganyika Daktari Alex Mrema amesema vifo hivyo vimetokea papo hapo, ambapo wanaume walikuwa watano kati yao kulikuwa na mtoto mmoja anayekadiriwa kuwa na umri miaka miwili.

"Wanawake wanne pia wamepoteza maisha wote watu wazima kati ya umri wa miaka 18 hadi 22 na mmoja mwenye umri kati ya 30 hadi 35 mwingine alikuwa mjamzito," amesema Mrema.

Aidha amesema kati ya majeruhi 30, baadhi yao wamepokelewa hospitalini hapo na wengine wanne wamepelekwa hospitali ya rufaa mkoa wa Katavi huku wengine wakitibiwa na kuondoka.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Ally Makame amethibitisha kutokea tukio hilo na kwamba wanaendelea kuchunguza chanzo cha ajali hiyo.

"Lakini tunatoa nasaha kwa madereva wetu kuwa makini na kuchukua tafadhari kubwa sana wanapopita kwenye milima hatarishi kama huu wa Nkondwe ni hatari mkoani kwetu," amesema Makame.

Naye Mkuu wa mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko amefika hospitali ya wilaya ya Tanganyika kutoa pole kwa wahanga.

"Nawapa pole wafiwa na majeruhi huduma zinaendelea kutolewa na utambuzi wa maiti utatolewa baadaye kupitia vyombo vya habari" amesema Mrindoko.

Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo, akiwemo Raphael Lutonja amesema alipigiwa simu kisha kupewa taarifa hizo na baada ya kufika eneo walikuta abiria wamekandamizwa wakaanza kuwanusuru.

"Baadhi yao walikuwa wamepoteza maisha, tunaomba serikali itusaidie hili eneo kwasababu ajali zinatokea mara kwa Mara," amesema Lutonja.

Mmoja wa Majeruhi wa ajali hiyo, Philberth Bugeraha aliyelazwa hospitali ya wilaya ya Tanganyika, amesema walipokaribia kwenye Kona hiyo gari lilikwenda kwa mwendo Kasi mithili ya breki kufeli.

"Kona ikishindikana ikapitiliza hadi shimoni, baadaye niliona kama giza nikafumbua macho nikaona nimeumia mkono nimo ndani gari lemeinama nikajikwamua kutoka," amesema Bugeraha.