Ajali ya ndege: Nini kinafuata?

Ndege ya Precision Air iliyopata ajali Ziwa Victoria Novemba 6, 2022 na kusababisha vifo vya watu 19 na majeruhi 24 ikitolewa kwenye maji.

Muktasari:

Waathirika wa ajali ya ndege ya Precision Air wanaweza kupokea angalau Dola 129,000 za Marekani (Sh300 milioni) kila mmoja ikiwa watafuata utaratibu unaofaa wa fidia kwa mujibu wa kanuni bora za kimataifa zinazoongoza sekta ya usafiri wa anga, wataalamu wamesema.


Dar es Salaam. Waathirika wa ajali ya ndege ya Precision Air wanaweza kupokea angalau Dola 129,000 za Marekani (Sh300 milioni) kila mmoja ikiwa watafuata utaratibu unaofaa wa fidia kwa mujibu wa kanuni bora za kimataifa zinazoongoza sekta ya usafiri wa anga, wataalamu wamesema.

Ndege hiyo 5H-PWF, ATR 42- 500 yenye uwezo wa kubeba abiria 48, iliyokuwa na abiria 39 (watu wazima 38 na mtoto mmoja) na wafanyakazi wanne, ilianguka katika Ziwa Victoria Jumapili saa 02:53 asubuhi ilipokuwa ikitokea Dar es Salaam kwenda Bukoba, mkoani Kagera.

Katika tukio hilo, watu 24 waliokolewa na wavuvi waliokuwa kwenye shughuli zao eneo hilo, hata hivyo watu wengine 19 walifariki dunia kwenye ajali hiyo na kusababisha simanzi kwa ndugu, jamaa na marafiki.

Mwenyekiti wa Chama cha Kampuni za Bima Tanzania, Khamis Suleiman alisema kwa kuzingatia kanuni za uwajibikaji, ndugu wa kila mtu anayefariki dunia katika ajali hiyo ya ndege anastahili kulipwa Dola 129,000 za Marekani.

“Kwa sheria za uwajibikaji, kama ilivyoelezewa kwenye mikataba ya usafiri wa anga, mtu anatakiwa kulipwa Dola 129,000,” Suleiman aliiambia Mwananchi, jana.

Alisema kiasi hicho kinaweza kuongezeka, kama waathirika watakuwa huru kwenda mahakamani kudai fidia kulingana na kiwango cha uharibifu ambao wanaweza kudai katika mchakato huo.

“Unazungumzia tukio ambalo kulikuwa na wataalamu vijana waliokuwa ndiyo wameajiriwa. Ndugu zao watakuwa huru kuomba malipo kulingana na kiwango cha madhara kama yatakavyothibitishwa na mamlaka husika,” alissema Suleiman.

Pia, alisema kwa kuwa mfumo wa kuwekea bima ndege kwa kiasi kikubwa unatokana na utaratibu wa kurudisha bima kati ya kampuni ya bima ya ndani na ile ya nje, mapato ya ajali hiyo yatabaki ndani ya nchi.

Alisema wale waliopata majeraha katika ajali hiyo pia watakuwa huru kudai fidia ikiwa wanataka.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Allied Insurance Brokers Tanzania Ltd (AIBT), David Nolan alisema ni vigumu kubaini kiasi sahihi cha kulipwa fidia kwa waathirika wa ajali.

“Hakuna jibu ‘sahihi’ swali gumu sana hasa lile, lililojaa hisia,” aliiambia Mwananchi.

Awali, alisema bima za mashirika ya ndege zinaweza kutafuta suluhisho na familia za waathirika na kuzuia kesi ndefu za mahakamani na ada za kisheria.

Alisema hata hivyo, hiyo itahusisha wategemezi wa papo hapo tu na wenzi wa ndoa ambao watakuwa na haki ya madai.

“Hata hivyo, kama familia haijafurahishwa na ofa hiyo, wanaendelea kuwasilisha madai ya kisheria dhidi ya shirika la ndege au upande wowote wanaohisi kuhusika na hasara hiyo. Hii mara nyingi hufanywa kama hatua ya kitabaka; familia nyingi za waathirika hukusanyika,” alisema Nolan.

Alitolea mfano kutokana na hali kama hiyo, akisema familia za Ukraine kutoka Uholanzi zilipokea zaidi ya familia za watu wa China ambao pia walihusika katika ajali ya Shirika la Ndege la Malaysia.

“Kiasi cha fidia kinatofautiana sana kulingana na vigezo vilivyo hapo juu,” alisema.

Pia, alisisitiza kwamba ndege inayotoa huduma hata hivyo ina dhima “kubwa” ya kulipa kiasi chochote cha fidia hadi kikomo fulani bila kujali hasara.

Mkataba wa Montreal ni mkataba wa kimataifa uliotiwa saini mwaka 1999 ili kuanzisha uwajibikaji wa shirika la ndege katika matukio ya kifo au majeraha kwa abiria.

Ukomo wa uwajibikaji uliowekwa kwa mtoa huduma ni takriban Dola 145,000 za Marekani (Sh338.8 milioni). Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliridhia mkataba huo mwaka 2003.

Mkataba huo wa Montreal hata hivyo unatumika tu kwa usafiri wa kimataifa.

Safari za ndege za ndani zinasimamiwa na Kanuni za Usafiri wa Anga za Tanzania za mwaka 2008, chini ya Sheria ya Usafiri wa Anga ya Tanzania ya mwaka 1977.

Sheria hiyo inaweka kikomo cha uwajibikaji cha Dola 120,000 za Marekani (Sh279.79 milioni) kwa kila abiria.

Kwa upande mwingine, Mtaalam wa Bima ya Usafiri wa Anga, Panachelius Pancras alisema kuna sheria zinazosimamia sekta ya usafiri wa anga duniani kote iwapo ajali itatokea na jinsi waathirika wanapaswa kulipwa fidia.

“Jambo muhimu hapa ni kwamba wale wanaohitaji kulipwa wanapaswa kushirikiana na wataalamu wa bima ili kuwaelekeza jinsi ya kufanya malipo hayo,” alibainisha.

Alisema ajali za ndege ni ngumu katika fidia, akibainisha kuwa wanamazingira wanaweza pia kusema kuwa kulikuwa na umwagikaji wa mafuta na wanaweza kuhitaji kulipwa pia.

Alisema malipo hayo yanategemea jinsi waathirika watakavyotoa hati zinazoonyesha jinsi ajali hiyo ilivyowasababishia matatizo wao na familia zao, kwa mfano, jinsi walivyopoteza wanafamilia wenye matarajio makubwa ya baadaye kama madaktari na wengine.

Meneja Uhusiano na Mawasiliano wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (Tira), Eliezer Rweikiza alisema mdhibiti wa bima atashirikiana na watu waliopata ajali na waliopoteza wapendwa wao na kuhakikisha wanapata fidia kwa mujibu wa sheria.

“Ikitokea maafa, uchunguzi unafanywa kwanza na baada ya hapo hatua za bima hufuata. Tunasubiri mchakato ufanyike ili wote walipwe fidia ipasavyo,” alisema Rweikiza.

Kwa upande mwingine, Meneja wa Madai ya Bima, Michael Emmanuel alisema kwa mtazamo wa bima na maagizo ya Chama cha Kimataifa cha Usafiri wa Anga (IATA), kila shirika la ndege linatakiwa kuwa na bima kwa ajili ya ndege zitakazolipia biashara hiyo lakini pia kuwajibika kuwalinda watu wengine wanaoweza kupata hali ya kutokuwa na uhakika inayoletwa na misiba kama hiyo. Alisema mashirika ya bima yana jukumu kubwa la kutekeleza kwa kadiri hatua za kuboresha hatari zilivyohusika kabla ya kukabiliana na hatari za anga ndani ya nchi. Pia, alisema mfanyatathmini atalazimika kutathmini rekodi za matengenezo ya ndege.


Wafaransa wachunguza ajali hiyo

Serikali ilithibitisha jana tayari wataalamu kutoka Ufaransa wamefika na kuungana na wataalamu wao wa Tanzania kufanya uchunguzi wa chanzo cha ajali hiyo.

“Wataalamu wa ndani wameanza uchunguzi tangu jana (juzi) na wengine wamewasili kutoka Ufaransa (ambako ndege za ATR zinatengenezwa). Uchunguzi huo utahusisha kupata taarifa kutoka kwenye vinasa sauti ndani ya ndege.

“Wachunguzi wa ajali za ndege huwa hawapewi muda wa kumaliza japo uzoefu unaonyesha wanachukua kati ya mwezi moja hadi miwili,” Katibu Mkuu wa Uchukuzi, Gabriel Migire aliliambia Mwananchi.

Pia, alisema taarifa za awali zinaonyesha ajali hiyo ilisababishwa na hali mbaya ya hewa wakati wa kutua.

Hata hivyo, alisema uchunguzi wa kina, unaohusisha wataalamu wa Tanzania na Ufaransa, pia utahusisha kupata taarifa kutoka kwa ving’amuzi vya taarifa za ndege na vinasa sauti miongoni mwa mambo mengine.

Vyombo vya habari vya kimataifa viliripoti Jumatatu iliyopita kutoka Ofisi ya Uchunguzi na Uchambuzi wa Usalama wa Anga ya Ufaransa (Bea) pamoja na washauri wa kiufundi kutoka Kampuni ya Ndege ya ATR ya Ufaransa na Italia, walikuwa wakielekea Tanzania kusaidia katika uchunguzi huo.

Wakimnukuu msemaji wa Bea, vyombo vya habari viliripoti kuwa ofisi hiyo ilikuwa ikituma timu Tanzania pamoja na washauri wa kiufundi kutoka kampuni ya ndege ya Franco-Italia ya ATR.

Chini ya sheria za kimataifa, uchunguzi unaoongozwa na wenyeji kwa kawaida utajumuisha ushiriki wa mamlaka nchini Ufaransa, ambako ndege iliundwa na Canada ambako injini zake za Pratt & Whitney zilitengenezwa.