TCAA: Uwanja wa Ndege Bukoba upo salama

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania, Hamza Johari akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, kuhusu ubora wa uwanja wa ndege wa Bukoba pamoja na ajali ya ndege iliyotokea Kagera na kusababisha vifo vya watu 19. Picha na Michael Matemanga

Muktasari:

  • Siku nne tangu kutokea kwa ajali ya ndege ya Shirika la Ndege la Precision Air iliyosababisha vifo vya watu 19 huku 24 wakinusurika, Mkurugenzi mkuu wa TCAA, Hamza Johari amewataka Watanzania kutokuwa na hofu kuhusu Uwanja wa Ndege wa Bukoba.

Dar es Salaam. Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Hamza Johari amesema licha ya kutokea ajali ya ndege ya Precision Air bado Uwanja wa Ndege wa Bukoba upo salama na amewatoa hofu Watanzania wanaotumia usafiri wanaolekea mkoani humo.


Amesema ajali hiyo iliyotokea Novemba 6 mwaka huu baada ya ndege hiyo kuanguka Ziwa Victoria karibu na uwanja huo na kusababisha vifo vya watu 19 na 24 kunusurika ilikuwa bahati mbaya huku akisema katika sekta ya anga tukio lolote linalotokea ni funzo ili kuhakikisha halijitokezi kwa mara nyingine.


Johari ameeleza hayo leo, Jumatano Novemba 9, 2022 wakati akizungumza na wanahabari kuhusu masuala mbalimbali kiwemo majukumu ya kiufundi ya TCAA na ajali ya ndege ya shirika la Precision Air.


Amesema uwanja wa ndege wa Bukoba una urefu wa mita 1500 na upana wa mita 30, una uwezo wa kuhudumia ndege zenye uzito wa tani 29. Hamza amesema Precision ilikuwa uzito wa tani 18.3.


"Kampuni ya Precision imeanza kwenda Bukoba tangu mwaka 1992 ikianza na ndege ya abiria saba na mwaka 1996 wakaongeza nyingine ya abiria nane pamoja na kuwepo ya ziada ya abiria 11. Mwaka 1998 walikuja ma ndege ya kubeba abiria 18 huku mwaka 2008 walianza safari ya kubeba abiria wengi.


"Kama kiwanja cha ndege cha Bukoba ni hatarishi basi tungekuwa na mlolongo wa ajili kwa takwimu hizi. Mwaka 1980 Air Tanzania ilianza safari za kwenda Bukoba ikianza na abiria 19 na mwaka 2017 ikaendelea na safari.



"TCAA tusipoyaweka sawa haya mambo wasafiri wataamini uwanja wa Bukoba sio salama, sisi ni wajibu wetu kuwaeleza kwamba ni salama, ajali iliyotokea ni bahati mbaya tu," amesema Johari.


Juzi wadau mbalimbali wa sekta ya anga wakiwemo marubani na wahandisi wa ndege walivitaja viwanja vya ndege vya Bukoba na Arusha wakisema vinawapa ugumu wa kutua na kuruka kutokana na hali ya hewa inayojotokeza mara kwa mara,pia uwepo wa milima katika maeneo hayo