Ajali yaua watatu, wanne wajeruhiwa Pwani

New Content Item (1)

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani Pwani Piusi Lutumo akizungumzia tukio la ajali iliyotokea usiku huko Mbala Mkoani Pwani na kusababisha vifo na majeruhi,Picha na Sanjito Msafiri

Muktasari:

  • Watu watatu wamefariki na wengine wanne wamejeruhiwa kufuatia ajali ya magari yaliyogongana usiku wa kuamkia leo.

Kibaha. Watu watatu wamefariki na wengine wanne wamejeruhiwa kufuatia ajali iliyohusisha magari mawili yaliyogongana uso kwa uso Kijiji cha Mbala Vigwaza mkoani Pwani usiku wa Oktoba 23, 2023.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumanne Octoba 24, 2023 Kamanda wa Polisi mkoani Pwani, Pius Lutumo amesema kuwa chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa dereva wa gari dogo aina ya Toyota Kluger lililokuwa likitokea mkoani Iringa kuelekea Jijini Dar es Salaam

"Waliokuwa kwenye gari dogo walikuwa wanatoka Iringa kuelekea Dar es Salaam na huyu wa lori aina ya Scania alikuwa akitokea Dar es Salaam kuelekea mkoani Morogoro, lakini dereva wa gari dogo alikuwa na mwendo mkali bila kuchukua tahadhari," amesema.

Amewataja waliopoteza maisha kwenye ajali hiyo kuwa ni pamoja na Mbuma anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka (35-40), Pokera (19) wote wakazi wa Mbezi Dar es Salaam na Mwanahamisi (18) mkazi wa Kijitonyama jijini humo.

Amewataja pia majeruhi kuwa ni pamoja na Amina Kondo mkazi wa Manzese Dar es Salaam, Abdallah Ally na majeruhi wawili ambao bado hawajatambulika majina yao.

Lutumo amesema kuwa miili ya marehemu hao imehifadhiwa kwenye Hospitali ya Lugoba na majeruhi wanaendelea kupatiwa matibabu kwenye Hospital ya Msoga mkoani Pwani.