Ajenda nyuma ya uzio wa mabati

Unguja. Kwa kawaida kukiwa na mradi wowote wa ujenzi, hususan majengo makubwa, kisheria lazima eneo lizungushiwe uzio wa mabati.

Zipo sababu nyingi za kufanya hivyo lakini chache kati ya hizo ni pamoja na kuimarisha usalama kwa watu wanaozunguka eneo hilo, kuzuia  kupita au kuepusha usumbufu wa kuingiliana kati ya mafundi na watu wengine wasiohusika.

Tangu ilipoingia madarakani Serikali ya Awamu ya Nane inayoongozwa na Rais Dk Hussein Mwinyi, Zanzibar imekuwa katika mwonekano huo wa kuzungushiwa mabati katika maeneo, ikiashiria kuwa kuna ujenzi unaondelea ndani yake.

Hata hivyo, kutokana na hali halisi ilivyo zimeibuka kauli na hisia mseto ambazo kwa namna moja au nyingine, zimekuwa ni kama kukejeli au kubeza hatua hiyo, ikidaiwa kuwa nchi inachimbwa tu mashimo na kuzungushiwa mabati, basi. Jambo hilo lilifanya mabati kuwa msemo maarufu kisiwani hapa.

Haikuishia hapo, wapo waliokwenda mbali zaidi wakidai nchi itauzwa bila kujua kwa sababu baada ya kuzungushwa mabati kwenye maeneo, itakuja zamu ya kuizungusha nchi nzima mabati huku wananchi wake wakiuzwa bila kujitambua.

Mbali na kuzungushiwa mabati, zilitolewa hoja zingine kwamba miradi inayojengwa kwenye mabati hayo, mingi haizingatii utaratibu wa kutangaza zabuni za miradi hiyo, hivyo ni mbinu za kufanya ubadhirifu wa fedha za umma.

Kauli hiyo iliwahi kutolewa na baadhi ya viongozi wa Chama cha ACT Wazalendo kwa nyakati tofauti katika baadhi ya mikutano ya hadhara ya chama hicho.

Hata hivyo mara kadhaa Rais Mwinyi amekuwa anasema kauli hizo zinatolewa ili kumkatisha tamaa yeye na Serikali yake, huku akiweka msimamo kuwa harudi nyuma wala kusikiliza maneno ya wakosaji.


Kejeli zaanza kuyeyuka

Hatimaye mabati yameanza kufunguliwa na kuonyesha majengo makubwa ambayo si tu yameanza kuipamba Zanzibar katika mwonekano mpya, bali hatua hiyo inatajwa kuleta mabadiliko makubwa ya kiuchumi na kijamii kisiwani hapa.

Wakati Dk Mwinyi anaingia madarakani, Zanzibar haikuwa kama ilivyo sasa, kimwonekano imepiga hatua kila sekta na zaidi mandhari ya kisiwa hiki imebadilika.

Licha ya majengo ya Zanzibar kuwa katika namna ya pekee ya ujenzi, mengi yalikuwa yamechakaa kiasi cha baadhi kupromoka na mengine kuonekana kuwa magofu.

Hata baadhi ya ofisi za Serikali zilikuwa chakavu na zingine zikiwa hazina mabango ya kuzitambulisha na hata zile zilizokuwa na mabango hayo yalikuwa yamechakaa.

Hali hiyo sasa inaanza kupotea na Unguja kuwa mji wa kisasa wenye majengo yanayoendana na sifa yake ya kuwa mji wa kitalii.

Dk Mwinyi alisema mwanzoni walipoingia madarakani mwaka 2021 walikuwa katikati ya kipindi kigumu cha Uviko-19 hakukuwa na fedha kabisa, hivyo miradi ya maendeleo haikufanyika.

“Mwaka uliofuata tukatekeleza miradi ya maji, shule za ghorofa kutokana na fedha za ahueni ya Uviko-19, zaidi Sh230 bilioni, tukawambia mmeona, sasa maji madarasa kila upande.

“Sasa mwaka huu tumefanya mara mbili ya Uviko-19, Sh460 bilioni tutaendeleza pale ambapo tuliishia ili mambo yote yakae sawa,” alisema.


Mabati au taratibu?

Baada ya kufanya hayo yote zimeibuka kauli mpya kwamba wanajenga miradi bila kufuata utaratibu, suala ambalo Serikali inasema hawana muda wa kupoteza kulisilikiza, bali “itaendelea kujenga miradi ya maendeleo na viwanja vya michezo, barabara za mijini na vijijini ili Zanzibar iwe kama Ulaya.”

Akizungumzia kuhusu maendeleo ya miradi hiyo, Waziri wa Nchi, ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi, Hamza Hassan Juma anasema kwa kiasi fulani mabati yameanza kufunguliwa na si kwamba yalikuwa yanafungwa kama fasheni, bali ilikuwa ni miradi mikubwa ya maendeleo.

“Kwenye hii miradi mabati tayari tumefungua, kinachoonekana sasa ni majengo ya shule, hospitali na masoko ya wajasirimali,” anasema Hamza.

Hata hivyo, Hamza anasema dhana ya kuzungushia mabati kwenye miradi ni mpya kwa Zanzibar, ndiyo maana wakati mwingine haikueleweka mapema kwa wananchi lakini sasa wanaanza kuona kilichokuwa ndani.

Anasema Serikali ilipoanza kuzungusha mabati, baadhi ya wananchi walianza kupiga kelele kwamba nchi itafunikwa lakini yanapoanza kufunguliwa, ndiyo wanaanza kuona maana ya mabati hayo.

Anasema katika mabati hayo zimejengwa shule kubwa za kisasa zenye ghorofa na zaidi ya vyumba 2,000 vya madarasa zimeshajengwa katika maeneo yaliyokuwa yamezungushiwa mabati katika mikoa yote za Unguja na Pemba.

Pia maeneo mengine zimejengwa hospitali kubwa za kisasa katika wilaya zote 11 za mikoa mitano ya Zanzibar.

Mbali na hospitali hizo, zinaendelea kujengwa hospitali mbili kubwa za mkoa ikiwemo ya Lumumba ambayo inatajwa miongoni mwa hospitali kubwa za kisasa Afrika Mashariki, ambayo inagharimu zaidi ya Sh22 bilioni.

“Ukiangalia katika utekelezaji wa ilani ya uchaguzi, iliahidiwa kwamba hospitali za wilaya zitafanyiwa ukarabati lakini Dk Mwinyi hakufanya ukarabati badala yake ameenda mbele zaidi ya ilani, kajenga upya,” anasema Hamza.

Kati ya hospitali hizo 11, moja ya Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba, imeshaanza kutumika huku zingine zikitarajiwa kuanza kufanya kazi hivi karibuni.

Kwenye mabati hayo, pia yanajengwa masoko makubwa matatu ya Mwanakwerekwe, Chuini na Jumbi ambayo ni mapya ya kisasa yenye ghorofa, ambayo yatawawezesha wajasirimali kuweka bidhaa zao na kuacha kuangaika mitaani.

“Wananchi wataondoka kutandika bidhaa zao kwenye magunia kwa hiyo wanakwenda kufanya shughuli zao katika mazingira mazuri ya kisasa yenye huduma zote muhimu,” alisema

Mbali na hayo, pia kila wilaya yamejengwa masoko mengine madogomadogo kwa ajili ya wajasiriamali, ili waweze kuendeshea shughuli zao katika maeneo rasmi.

Ndani ya mabati pia unafanyiwa ukarabati Uwanja wa Amani ambao kwa sehemu kubwa umevunjwa na kujengwa upya. Ulikuwa na uwezo wa kuchukua watu 12, 000 lakini ukarabati wake ukikamilika utaweza kuchukua watu zaidi ya 15,000.

Ukarabati huo unatajiwa kukamilika kabla ya Januari 2024 ili kuwezesha sherehe za miaka 60 ya Mapinduzi zifanyike humo.

Waziri Hamza anasema “hii kazi inayofanywa na Rais Mwinyi lazima tufike pahala tumpongeze kwani amefanya kazi kubwa na ya mfano.”

Said Hussein, mtaalamu wa masuala ya uchumi anasema wakati mabati hayo yakiondolewa kwa sasa matokeo ya mambo yote ni kuona huduma za kijamii zinakuwa bora zaidi kisiwani humo.

Akizungumzia ujenzi wa masoko mengi, anasema “hii ni faida kwao (wafanyabiashara) kwa sababu iwapo mtu akiwa na sehemu maalumu ya kufanya biashara hata kupata mkopo ni rahisi.  Hakuna mtu naweza kutoa mkopo wake kwa mtu ambaye hayuko sehemu maalumu ya kufanyia biashara kwa sababu wakati wowote anahama.”

Anasema wananchi watakuwa na uwezo wa kuendeleza ushirika wakiwa katika mwavuli mmoja kwa hiyo mjumuiko wa yote haya unaenda kuleta huduma bora kwa wananchi.

Ili kuleta tija katika mipango hiyo, wananchi wanashauriwa waunge mkono jitihada Serikali yao na kuhakikisha wanaimarisha amani na utulivu baada ya kuondoka siasa za mgawanyiko.