Ajinyonga kwa wivu wa mapenzi akiwa na ujauzito wa miezi tisa

Ajinyonga kwa wivu wa mapenzi akiwa na ujauzito wa miezi tisa

Muktasari:

  • Mwanamke mmoja amejinyonga kwa kutumia kanga kwenye mti wa mwembe katika kijiji cha Itununu wilayani hapa, kwa madai ya wivu wa mapenzi, huku akiwa na mimba ya miezi tisa.
  • Hilo ni tukio la pili la watu kujinyonga katika mazingira ya utata

Serengeti. Mwanamke mmoja amejinyonga kwa kutumia kanga kwenye mti wa mwembe katika kijiji cha Itununu wilayani hapa, kwa madai ya wivu wa mapenzi, huku akiwa na mimba ya miezi tisa.

Hilo ni tukio la pili la watu kujinyonga katika mazingira ya utata.

Januari 5, saa 11 jioni mwaka huu, Buroi Motera (38) mkazi wa kijiji cha Masangura alijinyonga kwa kamba pembeni mwa nyumba yake, akidaiwa kukwepa hukumu ya kesi ya jinai namba 115/2020 ya wizi wa mifugo iliyokuwa itolewe Januari 11, mwaka huu.

Mkuu wa wilaya ya Serengeti, Nurdin Babu alithibitisha Mkami Nyamhanga (21) kujinyonga Januari 17 kwenye mti wa mwembe uliopo shambani.

Alisema mwili wake ulionwa na watoto waliokuwa wanakwenda kuangua matunda kwenye mwembe huo na ndio waliotoa taarifa ya kifo hicho.

Kwa mujibu wa Babu, marehemu inadaiwa alikuwa anamtuhumu mume wake kuwa na mpenzi mwingine.

”Asubuhi alitoka bila kuaga mpaka alipogundulika amejinyonga kwa kutumia kitanzi cha nguo ambayo alifunga kwenye tawi la mwembe na kuning’inia,”alisema na kuongeza:

“Mganga aliyefanya uchunguzi alibaini kuwa kifo chake kimetokana na kitanzi shingoni kilichosababisha mzunguko wa damu na hewa kukosekana, ndugu walikabidhiwa mwili kwa ajili ya kuuzika na hakuna mtu aliyekamatwa lakini uchunguzi unaendelea.’’

Mganga mfawidhi wa zahanati ya Itununu, Melick Salapioni alilieleza Mwananchi kuwa mwanamke huyo alikuwa na mimba inayokaribia miezi tisa.

Alisema kutokana na mama kujiua, alikata mawasiliano ya hewa ya oksijeni kati yake na mtoto na hivyo kusababisha kichanga hicho kufa.

Akizungumzia suala la kuwatenganisha mama na mtoto, Dk Salaponi alisema kuwa inapotokea hivyo huwa hawaziki pamoja, ila kuna taratibu za kimila ambazo huandaliwa kwa ajili ya kuwatenganisha.

Hata hivyo, Mwananchi ilithibitishiwa kuwa upasuaji ulifanywa na mtu mmoja kijijini hapo ambaye inadaiwa aliwahi kufanya kazi katika hospitali ya Nyerere Mugumu.

“Alifanyia upasuaji ndani ya nyumba ya marehemu na kutoa mtoto wa kike ambaye alikuwa ameshaota nywele. Kwa kifupi, alikuwa amebakiza muda mfupi kujifungua. Yeye na mama yake watawekwa ndani ya jeneza moja na tutamzika ndani ya kaburi moja,” alisema mtoa taarifa mmoja ambaye hakutaka jina lake litajwe.

Mwenyekiti wa serikali ya kijiji hicho, Samwel Maitarya alisema baada ya taratibu za kimila kufanyika, waliwazika ndani ya kaburi moja mama na mtoto wake.