Akaunti za THRDC zafunguliwa baada ya miezi nane

Akaunti za THRDC zafunguliwa baada ya miezi nane

Muktasari:

  • Bodi ya Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) imetoa shukrani za dhati kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa uongozi wake unaojali na kuzingatia haki za binadamu na utawala bora, baada ya akaunti za mtandao huo zilizofungiwa kwa takribani miezi minane kufunguliwa.

Dar es Salaam. Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) umesema akaunti za benki za mtandao zilizofungwa kwa takribani miezi minane zimefunguliwa.

THRDC imetoa shukrani kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa uongozi wake unaojali na kuzingatia haki za binadamu na utawala bora.

Taarifa hiyo imetolewa leo Jumatano Aprili 21, 2021 na bodi ya mtandao huo na kutoa shukrani kwa wahisani, taasisi mbalimbali na wanachama walioshiriki kwa namna mbalimbali kuhakikisha mtandao unaendelea kutekeleza majukumu yake pia kuhakikisha kuwa changamoto husika zinatatuliwa.

Taarifa hili imeeleza kuwa kufunguliwa kwa akaunti hizo kumetokana na maelekezo kutoka kwa mamlaka za Serikali zilizoagiza kufungwa ili uchunguzi wa tuhuma ufanyike na kisha kutoa maelekezo kuwa zifunguliwe.

“Kufungwa kwa akaunti hizo tangu Agosti 2020 hadi sasa, kulisababisha mtandao kushindwa kutekeleza sehemu kubwa ya majukumu yake kwenye miradi ya utetezi wa haki za binadamu kama ilivyokuwa imeainishwa kwenye mipango yake ya 2020,” imeeleza taarifa hiyo.

Vilevile, Bodi imewashukuru watendaji na wafanyakazi wote wa mtandao kwa kujitolea kuendelea na majukumu yao na uvumilivu waliouonyesha kipindi chote cha changamoto ya kutokuwepo kwa fedha za mtandao.

“Bodi ya mtandao inapenda kuwashukuru wafadhili wa mtandao. Kwa kipekee, Bodi ya mtandao inamshukuru Samia kwa uongozi wake unaojali na kuzingatia haki za binadamu na utawala bora.

“Mtandao unaahidi kuendelea kufanya kazi kwa ukaribu na kwa kushirikiana na wadau na viongozi mbalimbali, mamlaka za Serikali, asasi za kiraia, mahakama, tume ya haki za binadamu, wadau wa maendeleo, vyombo vya habari, wanasheria, taasisi za kitaaluma, ofisi ya msajili wa asasi za kijamii na wanachama wake ili kuhakikisha kuwa utetezi wa haki za binadamu unafanyika kwa ufanisi na weledi mkubwa hapa nchini,” imebainisha taarifa hiyo.

Aidha imeeleza kuwa mtandao utaendelea kufanya kazi bila hofu kwa kuzingatia sheria, kanuni, miongozo na taratibu zote zilizowekwa na mamlaka zote ikiwemo ofisi ya uratibu wa mashirika yasiyokuwa ya kiserikali ili kuendelea kudumisha na kuboresha ushirikiano katika kazi za utetezi wa haki za binadamu.