Alex Msama akamatwa na Polisi ofisini kwa Waziri Silaa

Mkurugenzi wa Kampuni ya Udalali ya Msama Promotion, Alex Msama

Muktasari:

  • Alikuwa ofisini kwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Dar es Salaam. Mkurugenzi wa Kampuni ya Udalali ya Msama Promotion, Alex Msama, anashikiliwa na Polisi jijini hapa.

Kwa mujibu wa video iliyowekwa kwenye mtandao wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC Digital), Msama amekamatwa akiwa ofisini kwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Jerry Silaa.

Video hiyo inamwonyesha Silaa akiwa ameketi akitoa maelekezo kwa askari Polisi mwenye sare kumkamata Msama.

Silaa amesikika katika video hiyo akiuliza iwapo askari huyo ana pingu akajibiwa zipo chini.

Msama aliyekuwa amevaa fulana yenye mistari na koti lenye rangi ya kaki, ameonekana akiingia na askari kwenye gari dogo lenye rangi nyeusi lililokuwa limeegeshwa nje ya geti la jengo la Wizara ya Ardhi, lililopo Kivukoni jiji hapa.

Mbali na video hiyo, taarifa kutoka kwa watu walio karibu na Msama zimesema amekamatwa leo saa 10.00 jioni.

Mwananchi Digital imemtafuta Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro kwa simu, ambayo ilipokewa na msaidizi wake aliyeeleza yuko kikaoni.

Juhudi za kupata taarifa kutoka Jeshi la Polisi zinaendelea.

Ingawa haijawekwa wazi sababu ya kukamatwa kwa Msama, hivi karibuni Waziri Silaa alikaririwa na vyombo vya habari akimuhusisha na utapeli wa ardhi.