Advertisement

Alichokisema Maalim Seif kuhusu Serikali ya umoja wa kitaifa Zanzibar

Saturday November 21 2020
By Bakari Kiango

Ni ukweli usiopingika kuwa  kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar sasa limebakia kwa ACT-Wazalendo baada ya Rais Hussein Mwinyi kukiandikia barua ya kutaka jina la Makamu wa Kwanza wa Rais na kutentenga nafasi mbili za uwaziri kwa chama hicho.

Wakati ukweli ukiwa huo,  mwenyekiti wa chama hicho,  Maalim Seif Sharif Hamad ambaye aliwania urais Zanzibar katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 28, 2020 amesema bado wanatafakari kuhusu suala hilo.

maamilpic1

Maalim Seif Sharif Hamad

Awali ACT ilikataa kutambua matokeo ya Uchaguzi Mkuu huo kikidai kuchezewa rafu, lakini Maalim Seif  alipata zaidi ya asilimia 10 za kura zinazokipa chama hicho nafasi ya kushiriki kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa, kwa mujibu wa katiba.

Jana, Rais wa Awamu ya Nane, Dk Mwinyi aliwaambia waandishi wa habari wakati wa kutangaza baraza la mawaziri kuwa ametimiza utashi wa kikatiba wa kukiandikia chama kilichopata kura zinazotakiwa ili kitoe jina la mtu atakayeshika nafasi ya Makamu wa Kwanza wa Rais na ameacha nafasi mbili za uwaziri kwa ajili ya chama hicho.

“Tumepokea barua kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na tunaifanyia kazi,” alisema Maalim Seif jana.

Advertisement

Alipoulizwa kama wapo tayari kushiriki kuunda SUK, Maalim Seif alisema bado wanatafakari.

“Chama hakijafanya uamuzi, kiko katika hatua ya mashauriano. Pia chama kipo katika hatua ya mashauriano kuhusu waliopewa ubunge, uwakilishi na udiwani kwenda kula kiapo au la,” alisema Maalim Seif.

Alipoulizwa kama atakubali ikiwa atateuliwa kushika nafasi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif alisema: “Nitaheshimu maamuzi ya chama.”

ACT-Wazalendo imepata wawakilishi wanne, lakini wamebakia watatu baada ya mwakilishi mteule wa Pandani, Abubakar Khamis Bakary kufariki dunia hivi karibuni.

Katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya mwaka 2010-15 iliyongozwa na Dk Ali Mohamed Shein akiwa Rais, Maalim Seif alikuwa Makamu wa Kwanza wa Rais baada ya chama chake cha zamani chas CUF kupata zaidi ya asilimia 10 za kura.

Pia chama hicho kiliongoza Wizara ya Afya iliyokuwa chini ya Juma Duni Haji, Biashara na Viwanda (Nassor Mazrui), Elimu (Zahra Hamad) na Wizara ya Nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais (Fatma Ferej).

Hata hivyo, umoja huo ulianza kulegalega mwishoni mwa muhula huo na hali ikawa mbaya zaidi baada ya matokeo ya Uchaguzi wa Rais na wawakilishi kufutwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), iliyoamuru urudiwe na hivyo CUF kuususia.

Kutokana na CUF kuususia, hakuna chama cha upinzani kilichopata zaidi ya asilimia 10 ya kura za urais na hivyo Dk Shein kulazimika kuendeshas serikali bila ya Makamu wa Kwanza wa Rais, huku akimteua Hamad Rashid Mohamed wa ADC kuwa Waziri wa Kilimo na baadaye akawa Waziri wa Afya.

Mwingine ni Said Soud Said wa chama cha AAFP, aliyekuwa waziri asiyekuwa na wizara maalum.

Advertisement