VIDEO: Rais Mwinyi ateua mawaziri wake 12

Dk Mwinyi awaandikia barua ACT-Wazalendo kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa

Muktasari:

Rais wa Zanzibar Hussein Mwinyi ameteua mawaziri 12 huku akiacha nafasi mbili kwa Chama cha ACT -  Wazalendo.

Dar es Salaam. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi leo Alhamisi Novemba 19, 2020, ameteua mawaziri watakaokwenda kuongoza Wizara 12 kati ya 14 alizoziunda huku akiacha nafasi mbili wazi.

Akizungumza kutoka Ikulu ya Zanzibar katika matangazo yaliyorushwa moja kwa moja na televisheni ya Shirika la Utangazi la Tanzania (TBC), Rais Mwinyi alisema ameongeza Wizara moja katika Ofisi ya Rais.

“Ofisi ya Rais, badala ya kuwa na mawaziri watatu kama mwanzo, sasa ofisi ya Rais itakuwa na mawaziri wanne,” amesema.

Amesema Waziri wa kwanza atakuwa akishughulikia Uchumi na Uwekezaji.

“Kama nilivyosema katika hotuba yangu ya kufungua Baraza la Wawakilishi, nilieleza umuhimu wa sekta binafsi, kwa hiyo atashughulikia sekta binafsi, uwekezaji na diaspora,” alisema Rais Mwinyi.

Katika Wizara hiyo amemteua Nudrin Ramadhani Soraga kuiongoza.

Ametaja Wizara ya pili ya Ofisi ya Rais kuwa ni ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais tawala za Mikoa na Idara Maalumu za SMZ, ambayo amemteua Masoud Ally Mohamed kuwa Waziri wake.

Wizara ya tatu katika Ofisi ya Rais ni ya Ofisi ya Rais, Utumishi, Sheria na Utawala bora akisema ameziunganisha zilizokuwa Wizara ya Katiba na Sheria na Utumishi na Utawala Bora na Waziri wake atakuwa Haroun Ally Suleiman.

Rais Mwinyi pia ameiweka Wizara ya Fedha na Mipango kuwa moja kati ya Wizara zilizo chini ya Ofisi ya Rais huku akimteua Jamal Kassim Ally, kuwa waziri wake.

Katika ofisi ya makamu wa Rais, amesema kutakuwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi na hapo amemteua Khalid Salim Mohamed.

Pia, ametaja wizara nyingine ikiwamo ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo huku akimteua Soud Nahodha Hassan kuwa Waziri.

“Kwenye hili tumeondoa Uvuvi kwa sababu tunataka tuipe mkazo wa peke yake,” amesema Rais Mwinyi.

Kutokana na kuondolewa huko kwa Uvuvi, Rais Mwinyi ameunda Wizara mpya ya Uchumi wa Bluu na Uvuvi na  amemteua Abdallah Hussein Kombo kuwa Waziri wake.

Nyingine ni Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali itakayoshikiliwa na Simai Mohamed Said, huku akiunda Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ambayo Tabia Mwita Maulid atakuwa Waziri wake.

“Habari nimeitoa kwenye utalii nimeiweka hapa ili utalii tuupe mkazo unaostahili,” amesema.

Kutokana na kuondolewa huko, Rais Mwinyi pia ameunda  Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale ambayo Leila Mohamed Mussa atakuwa Waziri wake.

 Wizara nyingine ni pamoja na Ardhi na maendeleo ya Makazi ambayo Waziri wake atakuwa Riziki Pembe Juma.

Katika wizara hiyo ameondoa Maji na Nishati akisema ilikuwa kubwa sana.

“Ilani ya CCM tumeahidi mambo mengi kwenye maji na Nishati, kwa hiyo kuiweka pamoja inakuwa kubwa mno. Nimeamua kuzifanya mbili,” amesema. 

Nyingine ni Ujenzi Mawasiliano na Uchukuzi inabaki kama ilivyo aliyomteua Rahma Kassim Ally kuwa waziri wake na Wizara ya Nishati Waziri ambayo Suleiman Masoud Makame ameteuliwa kuwa Waziri wake.

Wizara zilizobaki wazi ni pamoja na Wizara ya Afya, ustawi wa Jamii Jinsia na Watoto na Wizara ya Maendeleo ya Viwanda akisema ni kwa sababu chama cha ACT Wazalendo kinachotakiwa kuingia kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa hakijapeleka majina.

“Kwa mujibu wa Katiba, mdau wa nafasi kwenye baraza la mawaziri, itategemea uwiano wa idadi ya viti vya wawakilishi kuchaguliwa.

“Kwa maana hiyo, ACT Wazalendo wana idadi ya viti vya Wawakilishi wa kuchaguliwa na ndiyo amana nimeacha nafasi mbili endapo watakuwa tayari,” amesema Rais Mwinyi.