Alichokisema Magufuli kuhusu ushirikiano wa Dk Mwinyi, Maalim Seif

Thursday January 14 2021
MAGUFULIPIC
By Aurea Simtowe

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania,  John Magufuli amesema mwanga wa maendeleo  Zanzibar umeanza kuonekana kutokana na umoja na kufanya kazi pamoja kati ya Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi na makamu wake, Maalim Seif Sharif Hamad.

Kiongozi mkuu huyo wa nchi ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Januari 14, 2021 wakati akizungumza na viongozi hao waliopo katika ziara ya siku mbili wilayani Chato Mkoa wa Geita

Amesema hilo lilimfanya akubali kutembelewa na Dk Mwinyi aliyeambatana na Maalim Seif kwa sababu aliona mwanga wa maendeleo ya Zanzibar ambao  unachangia  maendeleo ya Tanzania bara kwa sababu ni pande mbili za muungano zinazotegemeana.

“Kwa hiyo viongozi wote wawili hawa nimewaomba waendelee kuchapa kazi na mimi kama Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania nimewahakikishia ushirikiano, sitawaacha kamwe.”

“Hasa kwa sababu wote kwa umoja wao wanahubiri amani, Mwinyi anahubiri amani, Maalim Seif anahubiri amani, makamu wa pili anahubiri amani, Wazanzibari wote wahubiri amani,” amesema Magufuli.

Advertisement

Amebainisha kuwa zipo baadhi ya ndoa zilivunjika Pemba na pengine ni kwa sababu mwanamke aliipigia kura CCM na mwanaume kuchagua mgombea wa ACT-Wazalendo katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 28, 2020, “lakini siku ambayo Maalim Seif ameingiea serikalini ndoa zikaungana. Maamuzi yake yamewaunganisha wanandoa maana yake yana baraka kwa mwenyezi Mungu.”

Amesema mambo ya vyama hayapaswi kuwasumbua, “tunatakiwa Watanzania tutangulize maslahi ya mataifa yetu kwanza. Maadui zetu wangefurahi sana kuona tunagombana na Zanzibar inachafuka lakini wameshindwa kwa sababu viongozi nyie hamkuwa na mawazo ya kuvunja umoja wa kitaifa.”

“Ndiyo maana nawapongeza wewe Maalim Seif na Dk Mwinyi mmefanya lililo jema, mmewafanyia mema Wazanzibar na sasa mambo ya ubaguzi huyu mpemba huyu muunguja hayatakuwepo tena kama yatakuwepo ninyi mkahubiri huo umoja.”


Advertisement