Alikiba ni ngoma juu ya ngoma

Alikiba ni ngoma juu ya ngoma

Muktasari:

  • Msanii wa Bongofleva, Alikiba ameanza kutekeleza kile alichoahidi kwa mashabiki wake kuwa atakuwa anatoa nyimbo mfululizo hadi utakapofika wakati wa kuachia albamu yake ya tatu.

Dar es Salaam. Msanii wa Bongofleva, Alikiba ameanza kutekeleza kile alichoahidi kwa mashabiki wake kuwa atakuwa anatoa nyimbo mfululizo hadi utakapofika wakati wa kuachia albamu yake ya tatu.

Alikiba alikuwa amejijengea utamaduni wa kukaa muda mrefu bila kutoa wimbo jambo ambalo baadhi ya mashabiki wake walikuwa wakililalamikia.

Mathalani ilimchukua miaka miwili hadi pale alipokuja kuachia wimbo 'Seduce Me' ambao video ndio Ilikuwa ya kwanza nchini kupata watazamaji milioni 1 katika mtandao wa Youtube ndani ya saa 37 na kuivunja rekodi iliyokuwa inashikiliwa na video ya Diamond Platnumz 'Salome' iliyotumia saa 48 kupata idadi hiyo ya watazamaji.

Leo Alhamisi Juni 24, 2021 Alikiba ameachia wimbo uitwao Salute ambao amemshirikisha Rudeboy wa Nigeria aliyekuwa anaunda kundi la P Square.

Wimbo huo unakuja zikiwa ni takribani siku 14 tangu atoe wimbo mwingine. Juni 15, 2021 wa Ndombolo ambao amewashirikisha wasanii wote wa lebo ya Kings Music, Abdukiba, K2ga na Tommy Flavour.

Cover ya wimbo huu mpya (Salute) Alikiba na Rudeboy wanaonekana kuvalia mavazi ya kijeshi ingawa maudhui yake yanazungumzia mapenzi.

Alikiba anakuwa msanii wa pili Bongo kufanya kolabo na msanii wa P Square tangu kundi hilo kuvunjika. Wa kwanza ni Vanessa Mdee aliyemshirikisha Mr P kwenye wimbo wa Kisela.

Wakati P Square wakifanya vizuri Afrika, AY alikuwa msanii wa kwanza Tanzania na Afrika Mashariki kufanya nao kolabo.