Aliyefariki ajali ya ndege azikwa Arumeru

Muktasari:

  • Zaituni ni miongoni mwa watu 19 waliofariki dunia Novemba 6, 2022 baada ya ndege ya Precision Air kuanguka Ziwa Victoria karibu na Uwanja wa Ndege wa Bukoba mkoani Kagera.

Arumeru. Simanzi na majonzi vimetawala katika mazishi ya mmoja kati ya abiria 19 waliofariki katika ajali ya ndege iliyotokea Ziwa Victoria mkoani Kagera, Zaituni Mohamed Shillah (28).


Mazishi ya Zaituni yemefanyika leo Jumatano Novemba 9, 2022 katika eneo la TPRI wilayani Arumeru jijini Arusha.

Ibada ya mazishi ya Zaituni imeongozwa na Mchungaji Loserian Kambei wa Kanisa la The Mountain Hebron Ministry.



Zaituni ambaye alikuwa akifanya kazi jijini Dar es Salaam alifariki dunia wakati akiwa anakwenda kikazi mkoani Kagera.

Katika ibada hiyo iliyofanyika nyumbani kwa Idd wilayani Arumeru kabla ya kwenda kuzikwa katika eneo la TPRI, ilihudhuriwa na watu wachache.


Katibu Tawala wa Wilaya  ya Arumeru, James Mchembe, aliongoza waombolezaji katika mazishi hayo ambayo pia yalihudhuriwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Arusha, Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Suleiman Msumi, kamati ya ulinzi na usalama na ndugu na jamaa wa karibu wa familia hiyo.


Zaituni ambaye alizaliwa mkoani Dodoma Novemba 9, 2022, alikuwa akijishughulisha na kazi ya ofisa masoko wa kidigitali jijini Dar es Salaam.

Akihubiri katika ibada hiyo ya maziko, Mchungaji Kambei, amesema ajali hiyo imekuwa pigo kubwa kwa taifa kwani imepoteza nguvu kazi ambayo ilikuwa ikitegemewa


Kuhusu vijana alisema ni wakati wa jamii na taifa kwa ujumla kuombea kundi la vijana ambalo kwa asilimia kubwa wamekiuka maadili na kujihusisha na vitendo viovu.



"Tunalia kama kanisa, watu wanapenda anasa kuliko Mungu,vijana wanajishughulisha na matukio ya ajabu ikiwemo panya road,taifa linaelekea wapi?


"Wazazi tuombe kwa ajili ya vijana,watu wamejisahau, tunalia juu ya vijana ni lazima kama jamii tukemee vitendo viovu kwani kizazi kinaangamia,msiba huu ni huzuni kwani leo tunamzika Zaituni na ingekuwa maadhimisho ya siku yake ya kuzaliwa,"aliongeza



Kuhusu mvuvi Jackson Majaliwa, ambaye aliokoa manusura wa ajali hiyo ambaye alitumia kasia kuufungua mlango wa ndege  na kuwezesha watu 24 kuokolewa, amesema ni muhimu jamii kuhakikisha inatenda mema na kusaidiana bila kujali hali zao.


"Jiulize kijana aliyefanya uokoaji ni kijana ni mdogo sana inawezekana alikuwa anatamani kuwa jeshi la uokoaji, lakini hakupata nafasi hiyo.Watu wanalia,yeye imekuwa fursa kwake dunia inamjua leo kwa alichokifanya,labda alikata tamaa lakini Mungu amemsaidia,"amesema