Simanzi yatawala wakipokea mwili aliyefariki ajali ya ndege

Muktasari:

  • Zacharia Mlacha ni miongoni mwa watu 19 waliofariki dunia Novemba 6, 2022 baada ya ndege ya Precision Air kuanguka Ziwa Victoria karibu na Uwanja wa Ndege wa Bukoba mkoani Kagera.

Dar es Salaam. Simanzi na majonzi vimetawala katika familia ya Mlacha ambao ni wakazi wa Ubungo Riverside, mtaa wa Kibangu jijini Dar es Salaam, hii ni baada ya kupokea mwili wa mpendwa wao Zacharia Mlacha aliyefariki dunia katika ajali ya ndege ndege ya Precision Air.

 Zacharia ni miongoni mwa watu 19 waliofariki dunia Novemba 6 baada ya ndege iliyokuwa ina watu 43 kuanguka katika Ziwa Victoria, ikiwa inatoka jijini Dar es Salaam kwenda Bukoba, ambapo katika ajali hiyo watu 24 walinusurika.

Zacharia ambaye alikuwa anafanya kazi katika Taasisi ya Usimamizi na Maendeleo ya Afya (MDH) alikua katika safari ya kikazi kuelekea mkoani Tabora.

Msemaji wa Familia ambaye ni kaka wa marehemu Dk Yoremin Mlacha anasema wakati Zacharia anasafiri hakumueleza mtu yoyote, kuwa atasafiri jambo ambalo siyo kawaida yake.

“Zacharia huwa anasema wakati anasafiri, lakini hadi alivyo safari hakusema chochote,” amesema.

Dk Mlacha amesema Zacharia wakati wa uhai wake alikuwa ni mtu wa watu, kwa kuwa alikuwa habagui nani rafiki, nani adui.

Kwa upande wake mama mzazi wa marehemu amesema Zacharia ambaye ni mtoto wake wa pili alikua anamtegemea katika kuwaunganisha ndugu zake kuhusu mambo ya familia.

Naye, Goodluck Lyatuu ambae ni Mkurugenzi wa Miradi katika Taasis ya MDH ameeleza kwamba Zacharia ameacha pengo lisilozibika katika taasisi yao, kwa kuwa alikuwa ni mtu mahiri katika kitengo cha mawasiliano.

“Zacharia alikuwa na jukumu la kuwasilisha taarifa kwa jamii kuhusu kazi ambazo shirika la MDH wanazifanya, alikuwa ni mtu wa tofauti maana alikua na malengo ya mbali,” amesema