Aliyehukumiwa kifo akidaiwa kumuua mkewe na kumtupa kisimani, aachiwa huru
Muktasari:
- Mahakama ya Rufaa ya Tanzania imefuta adhabu ya kunyongwa hadi kufa aliyokuwa amehukumiwa Masoud Othman Nzengi, baada ya kukutwa na hatia ya kumuua mkewe, Mariamu Bakari Matoja, na kumtupa kwenye kisima cha maji, baada ya Mahakama kubaini kuwapo kwa dosari za kisheria katika usikilizwaji wa kesi hiyo Mahakama Kuu ya Zanzibar.
Serengeti. Mkazi wa Mkoa wa Kusini Unguja, Masoud Othman Nzengi ameachiwa huru na Mahakama ya Rufaa Tanzania baada ya Mahakama hiyo kufuta hukumu ya kunyongwa hadi kufa aliyokuwa amehukumiwa kwa kosa la kumuua mkewe, Mariamu Bakari Matoja na kumtupa kwenye kisima cha maji, ikibaini kuwapo kwa ukiukwaji wa taratibu za kisheria katika usikilizwaji wa kesi hiyo.
Mahakama ilisema ukiukwaji huo uliufanya mwenendo mzima wa kesi kuwa batili, hivyo kufuta hukumu ya Mahakama Kuu ya Zanzibar iliyokuwa imempata Masoud na hatia ya mauaji.
Uamuzi huo ulitolewa Juni 29, 2026 na jopo la Majaji wa Rufaa, Barke Sehel, Issa Maige na Lameck Mlacha, walioketi Zanzibar na kuruhusu rufaa ya Masoud dhidi ya Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP).
Mahakama pia iliamuru Masoud aachiwe huru mara moja isipokuwa kama anashikiliwa kwa sababu nyingine halali kisheria.
Msingi wa rufaa
Masoud alikuwa ameshtakiwa kwa kosa la kumuua mkewe nyumbani kwao Kidimni, Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja, Desemba 23, 2020.
Kwa mujibu wa upande wa mashtaka, shahidi muhimu alikuwa mtoto wa miaka 13, mjukuu wa wanandoa hao, aliyedai alimwona mrufani akimkandamiza marehemu shingoni kwa kutumia rungu.
Shahidi huyo alidai alijificha kwenye migomba ya ndizi na baadaye akamwona mrufani akimbeba marehemu hadi kwenye kisima cha maji na kumtumbukiza humo, kabla ya kumweleza kuwa bibi yake alikuwa amekimbia.
Amedai hakutoa taarifa mara moja, bali aliendelea kucheza na watoto wenzake. Siku iliyofuata, mwili wa bibi yake ulitolewa kisimani na polisi baada ya taarifa kutolewa.
Mtoto wa marehemu naye alidai alikuta skafu na viatu vya mama yake karibu na eneo la tukio pamoja na dalili za mwili kuvutwa, jambo lililomfanya amshuku baba yake kutokana na migogoro ya mara kwa mara iliyokuwapo kati ya wazazi wake.
Kwa upande wake, Masoud alikana kuhusika na mauaji hayo akidai mkewe alitoweka nyumbani na baadaye kupatikana amefariki dunia. Alisema waliishi pamoja kwa miaka 33 kama mume na mke.
Pia, alidai alikamatwa, akateswa kwa siku nane na kushinikizwa kukiri kosa, lakini alikataa kwa kuwa hakuwa na hatia.
Aidha, alihoji uaminifu wa shahidi mkuu wa mashtaka akidai alikuwa na tabia mbaya, mwizi na mtumiaji wa bangi, hivyo ushahidi wake haukupaswa kuaminiwa.
Baada ya kupitia ushahidi, Mahakama Kuu ilimkuta na hatia ya mauaji na kumhukumu adhabu ya kifo kwa kunyongwa, hatua iliyomfanya kukata rufaa Mahakama ya Rufaa.
Sababu za rufaa
Katika rufaa hiyo, Masoud aliwasilisha sababu 24 za kupinga hukumu, zikiwamo hoja kwamba Jaji wa Mahakama Kuu hakuwapa wazee wa baraza maelekezo yote muhimu ya kisheria kabla ya kutoa maoni yao, jambo ambalo ni takwa la sheria katika kesi za mauaji.
Uamuzi wa Mahakama ya Rufaa
Mahakama ya Rufaa ilichunguza uhalali wa muhtasari uliotolewa kwa wazee wa baraza wakati wa usikilizwaji wa kesi Mahakama Kuu na kubaini kuwa haukuwa umeandaliwa kwa kuzingatia matakwa ya sheria.
Majaji wamesema Jaji alitoa muhtasari wa ushahidi, lakini hakueleza mafundisho muhimu ya kisheria yaliyotumika baadaye katika hukumu, ikiwamo kanuni ya mtu wa mwisho kuonekana na marehemu, pamoja na namna ya kutathmini ushahidi wa shahidi mmoja wa utambuzi wa kuona.
Mahakama ilieleza maelekezo hayo yalikuwa ya lazima ili kuwawezesha wazee wa baraza kutoa maoni sahihi na ya kujitegemea kabla ya jaji kutoa uamuzi.
Mahakama pia ilibaini kasoro nyingine baada ya mmoja wa wazee wa baraza kuondolewa katika usikilizwaji wa kesi kutokana na kutokuwapo kwake, lakini baadaye akaruhusiwa kurejea kushiriki bila amri ya mahakama kubadilishwa.
Jaji wa Rufaa Mlacha amesema mzee huyo wa baraza alishiriki kusikiliza mashahidi waliobaki na hata kutoa maoni kuhusu ushahidi wa shahidi wa kwanza ambao hakuwahi kuusikiliza alipokuwa hayupo mahakamani.
Kwa mujibu wa Mahakama ya Rufaa, hatua hiyo ilikuwa kinyume cha sheria na iliathiri uhalali wa mwenendo mzima wa kesi.
Mahakama ilikataa ombi la upande wa mashtaka la kurejesha kesi Mahakama Kuu kwa ajili ya kusikilizwa upya, ikisema kufanya hivyo kungeipa Jamhuri nafasi ya kuziba mapungufu yaliyokuwapo katika ushahidi wake.
Majaji wamesema ushahidi wa shahidi mkuu uliokuwa msingi wa hukumu ya awali ulikuwa na kasoro za kisheria ambazo zisingeweza kurekebishwa kwa kuamuru kesi ianze upya.
Kutokana na sababu hizo, Mahakama ya Rufaa ilifuta mwenendo wote wa kesi, ikaondoa hukumu ya hatia na adhabu ya kifo dhidi ya Masoud na kuamuru aachiwe huru mara moja, isipokuwa kama anashikiliwa kwa sababu nyingine halali kisheria.