Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Aliyehukumiwa kwa kupokea rushwa kumhamisha mwalimu akwaa kisiki

Muktasari:

  • Alitiwa hatiani na kuhukumiwa kulipa faini au kifungo jela kwa kupokea rushwa kufanikisha mchakato wa kumhamisha mwalimu kutoka Babati kwenda Mkuranga.

Dar es Salaam. Jitihada za mwenyekiti wa zamani wa Halmashauri ya Mkuranga mkoani Pwani, Juma Abeid kujinasua na adhabu ya kulipa faini ya Sh700, 000 au kifungo cha miaka minne jela, zimekwaa kisiki katika Mahakama ya Rufani Tanzania.

Mwaka 2021, Abeid alitiwa hatiani na Mahakama ya Wilaya Mkuranga kwa kosa la kupokea rushwa ya Sh440, 000 kutoka kwa Bashiru Chande ili aitumie kufanikisha mchakato wa kumhamisha mkewe kutoka Babati kwenda Mkuranga.

Mkewe, Husna Tegera aliyekuwa shahidi wa saba wa Jamhuri, alikuwa mwajiriwa wa Serikali akiwa mwalimu katika Halmashauri Wilaya ya Babati Mkoa wa Manyara. Ilidaiwa Abeid alitumiwa fedha hizo kupitia simu yake ya mkononi.

Baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote mbili, Mahakama ya Wilaya Mkuranga ilimtia hatiani na kumhukumu kulipa faini ya Sh700, 000 au kutumikia kifungo cha miaka minne jela, endapo angeshindwa kulipa faini hiyo.

Mshtakiwa hakuridhishwa na hukumu akakata rufaa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, ambako pia Jaji Emmanuel Ngigwana aliyeisikiliza rufaa hiyo aliitupa, akieleza upande wa mashitaka ulithibitisha shtaka hilo bila kuacha shaka.

Hakuridhishwa na hukumu akakata rufaa Mahakama ya Rufani Tanzania ambayo nayo katika hukumu iliyoitoa Agosti 15, 2024 ilifuta mwenendo mzima wa kesi ya rufaa katika Mahakama Kuu kutokana na dosari za kisheria.

Baada ya kufuta mwenendo huo, jopo la majaji watatu, Ferdnand Wambali, Lilian Mashaka na Benhaji Masoud walimtaka Abeid kukata upya rufaa Mahakama Kuu ya Tanzania, kama bado ana nia ya kuendelea kupinga kutiwa kwake hatiani.


Kosa la rushwa lilivyokuwa

Katika kosa lililomtia hatiani na kuhukumiwa adhabu hiyo, ilielezwa kati ya Januari mosi, 2019 na Julai 22, 2019 akiwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mkuranga, Abeid alijipatia fedha hizo kwa njia ya rushwa kutoka kwa Chande kupitia simu yake.

Katika usikilizwaji wa kesi hiyo, upande wa mashtaka uliita mashahidi wanane kuthibitisha shtaka, akiwamo Chande na mkewe, Husna.

Fedha hizo zilitumwa kupitia kwa wakala Pauline Mgunda aliyekuwa shahidi wa tatu wa Jamhuri na kwamba, mwenyekiti alimtambulisha Chande aliyekuwa shahidi wa pili kwa Ofisa Elimu wa Mkuranga aliyekuwa shahidi wa kwanza.

Katika ushahidi huo, shahidi wa sita, Paulina Masampala akiwa Ofisa Elimu wa Wilaya ya Babati, alieleza aliwahi kupigiwa simu na mtu ambaye hamfahamu akimwelezea kuhusu suala la kumhamisha Husna.

Hata hivyo, alisema hakuweza kusaidia kumhamisha mwalimu huyo kwa sababu Babati kulikuwa na walimu wachache wa sayansi katika shule nyingi za sekondari, hivyo isingekuwa busara kumhamisha mwalimu huyo kutoka Babati.

Shahidi wa nane, Beneth Kapinga ambaye ni Ofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Wilaya ya Mkuranga alisema kupitia upelelezi wao, alikuwa na maoni kuwa mwenyekiti huyo alikuwa amejihusisha na vitendo vya rushwa.

Katika utetezi wake, Abeid alikanusha tuhuma hizo na kuita mashahidi watatu kumtetea, lakini baada ya usikilizaji kukamilika, mahakama ilimtia hatiani na kumhukumu kulipa faini ya Sh700, 000  au la atumikie kifungo cha miaka minne jela, hukumu ambayo hakuridhika nayo.


Hoja za kisheria kortini

Katika usikilizwaji wa rufaa Mahakama ya Rufani, mwenyekiti huyo wa zamani wa halmashauri aliwakilishwa na wakili wa kujitegemea Daniel Ngudungi, huku Jamhuri ikitetewa na mawakili wa Serikali, Fidesta Uisso na Clarence Mosha.

Katika hoja za kuunga mkono rufaa hiyo, Wakili Ngudungi alikubaliana na hoja ya kisheria iliyoibuliwa na Wakili Uiso kuhusu dosari za kisheria zilizobainika katika mwenendo wa rufaa yake Mahakama Kuu.

Alieleza ingawa hakumwakilisha mrufani Mahakama Kuu, lakini alipopitia jalada halisi na kumbukumbu za rufaa mbele ya mahakama hiyo, amebaini hapakuwapo notisi ya kukata rufaa iliyokuwa imewasilishwa Mahakama Kuu.

Kwa mujibu wa wakili huyo, hiyo ni kwenda kinyume cha takwa la kifungu namba 361(1)(a) ya Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) na kuwa kukosekana kwa notisi hiyo, kunafanya mahakama isikilize rufaa isiyo sawa.

Kutokana na hilo, aliiomba mahakama itamke kuwa mwenendo wa rufaa katika Mahakama Kuu ulikuwa batili, hivyo mahakama ibatilishe mwenendo huo.

Mbali na kuomba jopo la majaji libatilishe mwenendo huo, aliwasihi waendelee kusikiliza rufaa ya mteja wake kwa kurejea upya mwenendo huo, kwa kuegemea sababu zao za rufaa hasa hoja ya upendeleo wa Hakimu wa Mkuranga.

Wakili Uisso kwa upande wake, aliungana na Wakili Ngudungi kuiomba mahakama ibatilishe mwenendo wa kesi ya rufaa Mahakama Kuu katika rufaa namba 41 ya 2021 na kusisitiza hapakuwepo notisi ya rufaa iliyowasilishwa ndani ya siku 10.

Hata hivyo, hakukubaliana na hoja ya kutaka Mahakama ya Rufani iendelee kusikiliza rufaa na baadaye kurejea mwenendo huo, badala yake aliiomba mahakama kubatilisha mwenendo wote wa kesi Mahakama Kuu.

Wakili Uisso alisema mrufani bado anataka kuendelea kupigania haki yake kupinga hukumu ya Mahakama ya Wilaya Mkuranga, basi afanye mchakato huo kwa mujibu wa sheria za rufaa zilizopo.


Hukumu ya majaji

Katika hukumu, majaji walisema wamepitia kwa umakini mwenendo wa kesi ya rufaa Mahakama Kuu na kwamba, wanakubaliana kuwa rufaa ya mrufani mbele ya Mahakama Kuu ilikuwa batili kutokana na kukosekana kwa notisi ya kukata rufaa.

Majaji hao walisema kilichopo katika mwenendo huo ni sababu za rufaa ambazo huwa zinawasilishwa ndani ya siku 45 tangu kutolewa kwa hukumu na adhabu lakini sheria inataka lazima kuwepo notisi ya maandishi ya nia ya kukata rufaa.

Walisema kwa masikitiko, Mahakama Kuu ilipitiwa na takwa hilo la kisheria la kutaka uwepo wa notisi ya kukata rufaa na kusema mahakama husikiliza rufaa pale inapokuwa iko sahihi kulingana na sheria za nchi.

Majaji walikataa hoja ya wakili wa mrufani kwamba licha ya mwenendo wa kile kinachoitwa rufaa katika Mahakama Kuu kufutwa, itumie mamlaka yake kusikiliza na kuamua kuhusu malalamiko dhidi ya Mahakama ya Wilaya Mkuranga.

Kwa mujibu wa majaji, baada ya kubatilisha mwenendo huo, ni hiyari ya mrufani kukata rufaa upya Mahakama Kuu kupinga hukumu ya Mahakama ya Wilaya Mkuranga kwa kufuata sheria zinazoongoza mchakato wa kukata rufaa.


Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.