Aliyekuwa mfanyakazi wa REA akwaa kisiki mahakamani
Muktasari:
- Katika hukumu iliyotolewa Juni 16, 2026 na jopo la majaji wa rufaa ambao ni Barke Sehel, Paul Kihwelo na Ubena Agatho, waliokuwa wakisikiliza rufaa hiyo ya madai namba 190/2025 na nakala yake kuwekwa kwenye tovuti ya Mahakama.
Arusha. Aliyekuwa mtumishi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Prosper Msellem amekwaa kisiki katika Mahakama ya Rufaa, baada ya mahakama hiyo kutupilia mbali rufaa yake na kuthibitisha uamuzi wa Mahakama Kuu uliokataa kumuongezea muda wa kufungua maombi ya mapitio ya mahakama kupinga kufukuzwa kwake kazi.
Katika hukumu iliyotolewa Juni 16, 2026 na jopo la majaji wa rufaa ambao ni Barke Sehel, Paul Kihwelo na Ubena Agatho,waliokuwa wakisikiliza rufaa hiyo ya madai namba 190/2025 na nakala yake kuwekwa kwenye tovuti ya Mahakama.
Jaji Agatho amesema Mahakama ilibaini kuwa Mahakama Kuu ilitumia ipasavyo mamlaka yake ilipokataa ombi la Msellem la kuongezewa muda wa kufungua maombi ya mapitio ya mahakama.
Imesema baada ya kupitia hoja za pande zote imebaini madai ya jumla kuwa alikuwa mgonjwa wa muda mrefu, hayatoshi kuhalalisha kuongezewa muda bila ushahidi unaoonyesha siku mahsusi ambazo mwombaji alishindwa kuchukua hatua kutokana na ugonjwa huo.
Msellem alihudumu katika taasisi mbalimbali za Serikali ikiwemo REA, alipokuwa mtakwimu mkuu wa daraja la pili na baadaye alihudumu kwa nafasi nyingine, akahamishwa ofisi na kurejea REA alipokuwa Mkurugenzi wa Sera na Utafiti wa Mipango.
Mwaka 2017 alipewa notisi na hati ya mashitaka ya kinidhamu ikiwemo usambazaji wa taarifa ambazo haziruhusiwi kwa mujibu wa Sheria na kufukuzwa kazi Januari 26, 2018 baada ya kukutwa na hatia ya makosa hayo.
Baadaye alikata rufaa katika Tume ya Utumishi wa Umma (PSC), lakini rufaa hiyo ilikataliwa Mei 2019, kabla ya uamuzi huo kuthibitishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Oktoba mwaka huohuo.
Baada ya kushindwa katika hatua hizo, alikusudia kufungua maombi ya mapitio ya mahakama, lakini alikuwa amechelewa kwa zaidi ya miaka minne na siku 169, hali iliyomlazimu kuomba kuongezewa muda.
Aliomba kuongezewa muda, lakini Mahakama Kuu ilikataa ombi hilo kwa maelezo kuwa hakutoa sababu za kuridhisha kuhusu ucheleweshaji huo.
Katika rufaa ya sasa, Msellem alidai kuwa Mahakama Kuu ilikosea kwa kushindwa kuzingatia madai yake kwamba haki yake ya kusikilizwa ilikiukwa wakati wa mchakato wa kinidhamu na pia kushindwa kuzingatia hali yake ya afya aliyodai ilichangia kuchelewa kwake kuchukua hatua za kisheria.
Uamuzi wa Mahakama
Majaji hao baada ya kupitia mwenendo na hoja za pande zote mbili, walieleza Mahakama hiyo imekubaliana na hoja za Serikali kwamba madai ya ukiukwaji wa haki ya kusikilizwa hayakuwa ya wazi kiasi cha kuhalalisha kuongezewa muda na kwamba suala hilo lingehitaji uchunguzi wa kina zaidi.
Mahakama pia imesema maamuzi ya REA na Tume ya Utumishi wa Umma hayakuwa maamuzi ya mwisho yanayoweza kupingwa moja kwa moja kupitia mapitio ya mahakama, bali uamuzi wa mwisho ulikuwa ule wa Rais.
Kuhusu hoja ya afya, Mahakama ilieleza kuwa sheria inamtaka mwombaji kueleza kwa kina kila siku iliyosababisha ucheleweshaji wa kufungua shauri.
Jaji Agatho amesema wamebaini kuwa Msellem hakutoa maelezo ya kutosha kuhusu vipindi kadhaa vya muda, ikiwemo kati ya Oktoba mosi, 2019 na Januari 20, 2020.
Amesema kwa kuwa madai ya jumla ya kuwa mgonjwa wa muda mrefu hayatoshi kuhalalisha kuongezewa muda bila ushahidi unaoonyesha siku mahsusi ambazo mwombaji alishindwa kuchukua hatua kutokana na ugonjwa huo.
“Dai la jumla la kuwa chini ya hali ya kiafya halitoshi isipokuwa kila siku ya kuchelewa ihesabiwe,” imeeleza sehemu ya hukumu hiyo.
Mahakama ilihitimisha kuwa Mahakama Kuu haikukosea katika matumizi ya mamlaka yake ya hiari na kwamba hakuna msingi wa kuingilia uamuzi wake.
"Tunadhani mrufani alipaswa kutoa maelezo yanayoungwa mkono na ushahidi kuhusu siku gani maalumu alizotumia katika kliniki na zile alizotumia katika mambo mengine. Kwa hiyo tunakataa hoja ya pili kwa kukosa msingi. Kwa ufupi tunaona rufaa hii haina msingi hivyo inatupiliwa mbali,” imeeleza sehemu ya hukumu hiyo.
Aidha, Mahakama haikutoa amri yoyote kuhusu gharama za kesi.