Aliyekuwa waziri wa utalii aburuzwa kortini kwa ufisadi

Waziri wa zamani wa Utalii nchini Kenya, Najib Balala, aliyekuwa katibu mkuu wake, Leah Adda Gwiyo na Joseph Odero wakiwa mahakamani leo, Desemba 22, 2023.

Muktasari:

  • Mradi wa Chuo cha Utalii Pwani wamponza, yumo pia aliyekuwa katibu mkuu wake na mkandarasi mshauri.

Mwanza. Waziri wa zamani wa Utalii nchini Kenya, Najib Balala na aliyekuwa katibu mkuu wake, Leah Adda Gwiyo wametiwa mbaroni kwa madai ya kukiuka taratibu za ununuzi wakati wa ujenzi wa Chuo cha Utalii Pwani, huko Kilifi.

Wawili hao wamefikishwa mahakamani mjini Mombasa leo Ijumaa Desemba 22, 2023, walitiwa mbaroni na maofisa usalama kutoka Tume ya Maadili na kupambana na Rushwa nchini Kenya (EACC), jana Alhamisi Desemba 21, 2023.

Kwa mujibu wa habari zilizochapishwa na mtandao wa gazeti la Nation la nchini Kenya pamoja na vigogo hao wa zamani wa Serikali, mshauri kutoka taasisi ya ujenzi, Joseph Odero naye ameshikiliwa na anatarajiwa kufikishwa mahakamani.

Balala, mmoja wa viongozi wenye ushawishi katika siasa za Kenya, hasa ukanda wa Pwani anakabiliwa na madai 10 yanayohusiana na malipo yenye utata wa Sh8.5 bilioni za Kenya (zaidi ya Sh137 bilioni za Tanzania) zilizotengwa kwa ajili ya ujenzi wa tawi la Chuo cha Utalii Kenya, eneo la Ukanda wa Pwani.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka EACCm zaidi ya Sh4 bilioni za Kenya (zaidi ya Sh65 bilioni za Tanzania) kutoka Mfuko wa Utalii zililipwa kwa kampuni ya Baseline Architech Limited ikiwa ni gharama za ushauri kwenye mradi wa ujenzi wa chuo hicho eneo la Vipingo, Kaonti ya Kilifi.

Balala na wenzake watakabiliwa na mashtaka matatu ya kukiuka makusudi sheria ya manunuzi, kujipatia au kujimilikisha mali ya umma, kinyume cha sheria na matumizi mabaya ya ofisi ya umma.

Uchunguzi wa gazeti la Nation umebaini kuwa kampuni ya Mulji Devral and Brother ndiyo iliyopewa kandarasi ya ujenzi wa chuo hicho ambacho awali ilikuwa chini ya Chuo cha Utalii Kenya, kabla ya kuhamishiwa Wizara ya Utalii enzi za uongozi wa Balala.

Kukamatwa kwa watatu hao kumekuja wiki mbili tangu EACC ilipokamilisha na kuwasilisha taarifa za uchunguzi Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (ODPP).

Inatarajiwa kuwa takriban watu 13 ambao bado hawajakamatwa watafikishwa mahakamani kwa tuhuma mbalimbali zinazohusiana na suala hilo la ujenzi wa Chuo cha Utalii Pwani ambacho sasa kinajulikana kama Chuo cha Utalii cha Ronald Ngala.

Mradi wa ujenzi wa Chuo cha Utalii cha Ronald Ngala katika ukanda wa pwani ya Kenya ulilenga kupunguza mzigo (wa wingi wa wanafunzi) katika kituo chake cha mjini Nairobi.