Aliyengolewa jino, kutobolewa jicho kuona tena

Jackline Mnkonyi (38), mkazi wa jijini Arusha anayedaiwa kung'olewa jino na kutobolewa jicho na mpenzi wake.

Muktasari:

  • Uchunguzi wa awali unaonyesha mwanamke Jackline Mnkonyi (38) mkazi wa Sombetini jijini Arusha, ambaye alitobolewa macho na kung'olewa jino, uwezo wake wa kuona haujaathiriwa kwani jicho moja halijaharibika.

Arusha. Uchunguzi wa awali unaonyesha mwanamke Jackline Mnkonyi (38) mkazi wa Sombetini jijini Arusha, ambaye alitobolewa macho na kung'olewa jino, uwezo wake wa kuona haujaathiriwa kwani jicho moja halijaharibika.

 Lakini hata lile linalosadikiwa kuchoma na kitu chenye ncha kali, halijaathiriwa uwezo wake kutokana na kwamba mboni ya jicho haikuathiriwa.

Akizungumza na mwananchi jana baba mzazi wa mwanamke huyo, Elimilis Mnkonyi alisema Jackline alifanyiwa uchunguzi Jana katika hospitali ya Kaloleni jijini Arusha na kubaini bado atakuwa na uwezo wa kuona.

"Jicho moja alichomwa kitu chenye ncha kali lakini haikutuboa mboni hivyo baada ya uchunguzi tumeelezwa ataona na jicho jingine pia halijaharibika sana," alisema.

Alisema baada ya uchunguzi wamepatiwa matibabu na wanaimani siku si nyingi uwezo wa kuona wa Jackline utarejea.

Akizungumzia jino alisema uchunguzi umebaini jino moja limengolewa wakati jingine limevunjika na kwamba Jackline ataendelea na matibabu ili kuondolewa jino lililovunjika.

Hata hivyo alisema kwa Sasa wanaiachia serikali kuendelea na uchunguzi baada ya kukamatwa kwa Mtuhumiwa.

"Mtoto ataendelea kuwa nyumbani akipata matibabu lakini mambo ya kesi tumeachia serikali na sisi tutakuwa mashahidi wa Jamuhuri," alisema.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha, juzi lilifanikiwa kumkamata Isaack Mnyangi (45) mkazi wa Sombetini jijini Arusha anayetuhumiwa kumjeruhi kwa kumng'oa jino na kumtoboa jicho Mkewe Jackline kutokana na wivu wa mapenzi.

Kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo, kulitokana na msako wa makachero wa Polisi na ndugu wa mwanamke ambaye amefanyiwa ukatili huo.

Kamanda wa jeshi la Polisi mkoani Arusha, Justine Masejo, alisema mtuhumiwa huyo alitiwa mbaroni juzi eneo la Himo mkoani Kilimanjaro alikokuwa amejificha kukwepa mkono wa sheria.

Kamanda Masejo alisema taratibu za kisheria zimeanza kuchukuliwa na jarada la kesi hiyo litafikishwa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka hata hivyo hadi Jana bado alikuwa hajafikishwa mahakamani.

Akizungumza nyumbani kwa wazazi wake eneo la Sinoni Daraja Mbili Jijini Arusha, Jackline ambaye ana mtoto mchanga, amesema alipigwa na mumewe baada ya kumtuhumu ana uhusiano wa kimapenzi na mgeni aliyefika nyumbani bila kujua kama ni mjomba wake.

Alisema kuwa, Mei 23, 2023 alitembelewa na Mjomba wake ambaye ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Simiyu, Vicenti Matai kwa lengo la kumsalimia.

Alisema alipoondoka, mumewe Isaack waliyezaa naye watoto wawili, alifika nyumbani na kuanza kumuhoji juu ya mgeni aliyefika nyumbani akitaka kujua alikuwa nani.

Jackline alisema alimweleza mumewe kuwa mgeni huyo alikuwa na mjomba wake lakini alikataa na ndipo alipoanza kumshambulia kwa ngumi, mateke na mkanda na baadaye alichukua plaizi na kumng'oa jino kwa nguvu.

"Nilijitahidi sana kujieleza lakini ilishindikana alianza kunipiga kwa mateke na ngumi na alichukua plaizi na kuniamuru nifungue mdomo na kuning’oa jino moja ambapo damu zilianza kuchuruzika na kuanguka chini," alisema.

Alisema licha ya kipigo hicho pia alichukua kitu chenye ncha kali na kumtoboa jicho moja ambalo hadi sasa hawezi kuona huku akimwambia maneno mazito na kumtishia kumuua.

Amesema baada ya tukio hilo alimchukiwa na na kumpeleka nyumbani kwa wazazi wake Sinoni Daraja mbili na kumtumpa getini.

‘’Nimetobolewa jicho na kung’olewa jino na plaizi nina maumivu makali sana naiomba serikali ichukue hatua dhidi ya mume wangu kwani amenifanyia unyama wa hali ya juu sana,’’ amesema.