Aliyeuawa kwa kukatwa panga azikwa kwa wazazi wake Moshi

Muktasari:
- Magreth Mushi (50) anayedaiwa kuuawa na kaka yake, Neoni Lazaro wakati wakigombania mauzo ya nyanya ya Sh40,000 amezikwa katika kijiji cha Singa Kibosho,Wilaya ya Moshi Mkoani Kilimanjaro kijijini kwa wazazi wake leo Februari 15.
Moshi. Magreth Mushi (50) anayedaiwa kuuawa na kaka yake, Neoni Lazaro wakati wakigombania mauzo ya nyanya ya Sh40,000 amezikwa katika kijiji cha Singa Kibosho,Wilaya ya Moshi Mkoani Kilimanjaro kijijini kwa wazazi wake leo Februari 15.
Magreth Mushi aliyekuwa akiishi kijiji cha Urauri kata ya Reha wilayani Rombo alifariki dunia Februari 10, mwaka huu baada ya kudaiwa kukatwa katwa na panga kichwani na kaka yake huyo ambaye alikuwa akiishi naye wilayani humo.
Akizungumza kwenye mazishi hayo, mtoto wa marehemu Francis Kisoka aliiomba serikali kumchukulia hatua kali Mjomba wake anayedaiwa kumuua mama yake ambaye alikuwa hana hatia.
"Nimeumia sana kumpoteza mama yangu jamani, naiomba serikali ichukue hatua kali dhidi ya mjomba wangu kwa kumuua mama yangu,walikuwa hawana ugomvi wowote ,yaani ugomvi wa nyanya za mama yangu alizolima? nasikitika mno," amesema mtoto huyo huku akitokwa na machozi
Naye Mwenyekiti wa kitongoji cha Singa chini, Pantaleo Kileo amesema kuwa kwa miaka mingi kijana huyo anayetuhumiwa kusababisha mauaji amekuwa ni tishio kwa wananchi na kuisumbua serikali ya Kijiji kwa muda mrefu.
"Huyu kijana amekuwa akisumbua sana hapa Kijijini na amekuwa akifanya matukio ya kutisha, amefanya watu vilema kwa kuwakata mikono na wengine kuwaua,watu hapa kijijini hawalali, tunapojaribu kumkamata na kumpeleka kwenye vyombo vya sheria tunashindwa kutokana na mbinu alizonazo," amesema Mwenyekiti huyo.