Anayedaiwa kujifanya wakili apandishwa kizimbani

Wanaodaiwa kusafirisha heroin kizimbani

Muktasari:

  • Baraka Mukama anayedaiwa kufanya kazi za uwakili bila kuwa na sifa, amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa mashitaka ya kufanya kazi hiyo kinyume cha sheria.

Dar es Salaam. Hatimaye, Baraka Mukama (45) anayedaiwa kujifanya wakili wa kijitegemea, amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kujibu mashtaka mawili ambayo ni kufanya kazi ya uwakili bila kuwa na sifa na kumzuia mtumishi wa umma asitimize majukumu yake.

Baraka ambaye ni mkazi Kigamboni, amefikishwa mahakamani hapo leo Jumatatu Oktoba 2, 2023 na kusomewa kesi ya jinai namba 177/2023.

Mshtakiwa huyo amesomewa mashtaka yake na wakili wa Serikal, Judith Kyamba, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Ushindi Swallo.

Itakumbukwa kuwa Mei 23, 2023 mshtakiwa huyo alizua tafrani na taharuki mahakamani hapo baada ya kuzuia askari Polisi waliokuwepo mahakamani hapo, wasiwakamate upya wateja wake (washtakiwa) ambao walikuwa wamefutiwa kesi yao.

Kutokana na tafrani hiyo, Mukama alikamatwa na kupelekwa kituo cha Polisi kwa ajili ya kuhojiwa na mara baada ya mahojiano, ilibainika kuwa Mukama sio wakili wa kijitegemea na wala hajawahi kuwa mwananchama wa Chama cha Mawakili Tanganyika( TLS).

Akimsomewa mashtaka yake, wakili Kyamba amedia katika shtaka la kwanza, Mukama anadaiwa kuzuia mtumishi wa Umma asitimize majukumu take ipasavyo, tukio analodaiwa kulitenda Mei 23, 2023 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu

Wakili Kyamba amedai, siku hiyo ya tukio, mshtakiwa kwa makusudi alimzuia askari polisi mwenye namba J515 PC Mubaraka Abdallah, asimkamate Harid Rajabu maarufu kama Somole, ambaye alifutuwa kesi ya jinai namba 99/2019.

Shtaka la pili ni kufanya kazi ya uwakili bila kuwa na sifa, tukio analodaiwa kulitenda Mei 23, 2023 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Mshtakiwa anadaiwa siku hiyo, akiwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Romuli Mbuya, mshtakiwa alijiwakilisha kama wakili wa kijitegemea mwenye namba ya usajili 4696, wakati akijua ni uongo na yeye sio wakili.

Mshtakiwa huyo alijiwakilisha kama wakili katika kesi ya jinai namba 99/2019 ambayo alikuwa anawatetea washtakiwa wawili kati ya wanne waliokuwa wanakabiliwa na mashtaka ya kughushi nyaraka na stika mbalimbali za dawa.

Mukama baada ya kusomewa mashtaka yanayomkabili, alikana kutenda makosa hayo na kuomba Mahakama impatie dhamana kwa kuwa mashtaka yanayomkabili yana dhamana.

Upande wa mashtaka umedai kuwa upelelezi umekamilika hivyo wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kumsomea mshtakiwa hoja za awali (PH).

Hakimu Swallo alitoa masharti ya dhamana dhidi ya mshtakiwa huyo, ambayo ni kuwa na wadhamini wawili wanaotambulika na wenye barua kutoka Serikali za Mitaa, watakaosaini Bondi ya Sh 1milioni kila mmoja.

Hata hivyo, mshtakiwa huyo yupo nje kwa dhamana baada ya kutimiza masharti.

Hakimu Swallo ameahirisha kesi hiyo hadi, Oktoba 16, 2023 kwa ajili ya mshtakiwa kusomewa hoja za awali.

Mukama anadaiwa kuleta tafrani hiyo ya kuzuia askari polisi wasikamate washtakiwa, Mei 23, 2023  muda mfupi baada ya wafanyabiashara, Khalid Somoe (54) mkazi wa Keko Mwanga, Raphael Lyimo (40), mkazi wa Kimara Bonyokwa, Betty Mwakikusye (41) mkazi wa Chanika Msumbiji na Abdiel Mshana (57) mkazi wa Msasani Ubalozini, kufutiwa kesi yao ya  jinai namba 99/2019 na Mahakama.

Katika kesi hiyo, washtakiwa hao walikuwa wanakabiliwa na mashtaka 16 yakiwemo ya kula njama na kughushi stika za dawa zilizokwisha muda wake kwa kuziongezea muda wa matumizi.

Kati ya mashtaka hayo 16, mashtaka 15 yalikuwa ya kughushi stika za dawa tu.


TLS yamkana

Baada ya kutokea kwa sakata hilo, Chama cha Wanasheria wa Tangangika (TLS) kimesema Mukama sio mwanachama wake na hajawahi kuwa mwananchama.

Baada ya kubainika Mukama sio mwanachama wa TLS, chama hicho kiliunda tume ya mawakili watano kuchunguza uhalali wa Mukama.