Anayedaiwa kuvamia kanisa amhoji padri ulipo ushahidi

Mshtakiwa Elpidius Edward (22) akiwa chini ya ulinzi akisubiri kurejeshwa mahabusu baada ya shauri la kuvamia na kuharibu mali ndani ya Kanisa kuu Jimbo Katoliki Geita kuahirishwa.

Muktasari:

Mshtakiwa Elpidius Edward mkazi wa Mtaa wa Katundu Wilaya ya Geita anayedaiwa kuvamia Kanisa Kuu la Kiaskofu jimbo Katoliki Geita na kufanya uharibifu uliosabisha hasara ya Sh48.2 milioni amemtaka shahidi wa tano katika kesi hiyo kuieleza Mahakama kwanini hakupeleka mahakamani hapo ushahidi wa kamera za CCTV alizomkuta akiharibu.

Geita. Mshtakiwa Elpidius Edward mkazi wa Mtaa wa Katundu Wilaya ya Geita anayedaiwa kuvamia Kanisa Kuu la Kiaskofu jimbo Katoliki Geita na kufanya uharibifu uliosabisha hasara ya Sh48.2 milioni amemtaka shahidi wa tano katika kesi hiyo kuieleza Mahakama kwanini hakupeleka mahakamani hapo ushahidi wa kamera za CCTV alizomkuta akiharibu.

Mshtakiwa huyo ambaye hana wakili alianza kumuuliza maswali shahidi huyo wa tano ambaye ni Padri Charles Kato wa kanisa katoliki jimbo la Geita mara baada ya kumaliza kutoa ushahidi wake aliokuwa akieleza Mahakama namna alivyomkuta mshatakiwa akifanya uharibifu ndani ya kanisa hilo.

Mshatakiwa huyo alihoji kama alimkuta akivunja CCTV Kamera kwanini hakuipeleka mahakamani kwa kuwa ndio ushahidi wenye uhalisia kuliko kuja mwenyewe kuieleza Mahakama.

Akijibu swali hilo Shahidi Kato amedai asingeweza kuleta ushahidi wa CCTV kamera kwakuwa tayari mshtakiwa aliharibu mfumo wa CCTV kabla ya kuifikia kamera.

Mshtakiwa huyo pia alitaka kujua mtu sahihi aliyefungua mlango wa kanisa kutokana na shahidi aliyetangulia kudai siku ya tukio yeye ndie aliyekuja na funguo na kufungua lango kuu la kanisa kisha walinzi kuingia na kumdhibiti na leo shahidi huyo anaeleza yeye ndie aliyefungua kanisa hilo.

Akijibu swali hilo Shahidi Kato amedai kuwa yeye alipita kwenye mlango wa ‘Sakristia’ (mlango wa pembeni) ulipo mtambo wa CCTV camera akiwa na walinzi wanne na ndipo alipomkuta akiharibu mfumo wa kamera za kanisa hilo.

Awali Shahidi huyo ambaye ni Padri wa jimbo Katoliki Geita ameieleza Mahakama kuwa usiku wa Februari 26, 2023 akiwa amelala alipigiwa simu na mlinzi na kumweleza kuna mtu ndani ya kanisa anayefanya uharibifu wa vifaa.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali, Godfrey Odupoy; Padri Kato ameieleza Mahakama kuwa baada ya kupokea simu alikwenda eneo la tukio alipofika alikutana na walinzi wengine wanne ambao aliingia nao ndani ya kanisa na kumkuta kijana huyo akifanya uharibifu na kufanikiwa kumdhibiti.

Ameieleza Mahakama kuwa baada ya kumdhibiti na kufanikiwa kumtoa nje walimpigia simu paroko wa kanisa aliyefika na kuwapigia simu polisi waliokuja na gari ya doria kisha kumchukua mshtakiwa.

Shahidi huyo alipoulizwa kama mshtakiwa alikuwa na zana zozote alizotumia kufanya uharibifu alidai hakuwa na chochote bali alitumia mikono yake.

Ameieleza Mahakama kuwa mbali na kufanya uharibifu kwenye eneo la CCTV Kamera mshatakiwa huyo alikuwa amevunja misalaba, Tebernaco, sanamu ya bikira maria.

Elpidius anashtakiwa kwa makosa mawili ikiwemo la kuingia katika jengo la Kanisa Katoliki Geita kinyume na kifungu cha 294 (1) na (2) cha kanuni ya adhabu sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022.

Katika shtaka la pili mshtakiwa huyo anashtakiwa kwa uharibufu wa mali kinyume na kifungu namba 226 (1) cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022 na kusababisha uharibifu wa mali zenye thamani ya Sh48.2 milioni.

Kesi hiyo inayosikilizwa na Hakimu Mwandamizi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Geita, Johari Kijuwile  imeahirishwa hadi Septemba 11 mwaka huu kwa upande wa mashtaka kuendelea kuleta mashahidi.