Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Anglikana walivyomuaga Askofu aliyefariki baada ya kuhubiri kanisani

Muktasari:

“Mwenyezi Mungu ana maajabu yake na ametuonyesha kwa Askofu George Chiteto. Ni siku sita tu alizotumikia uaskofu tangu alipochaguliwa kuwa askofu wa tatu wa Dayosisi ya Mpwapwa na mahubiri yake ya kwanza aliyatoa juzi Jumamosi na ndiyo ikawa ni mahubiri ya kutuaga.”

Muheza. “Mwenyezi Mungu ana maajabu yake na ametuonyesha kwa Askofu George Chiteto. Ni siku sita tu alizotumikia uaskofu tangu alipochaguliwa kuwa askofu wa tatu wa Dayosisi ya Mpwapwa na mahubiri yake ya kwanza aliyatoa juzi Jumamosi na ndiyo ikawa ni mahubiri ya kutuaga.”

Hayo ni maneno aliyoyasema Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dk Maimbo Mndolwa alipokuwa akitoa mahubiri kwenye Misa ya kuuaga mwili wa Askofu Chiteto iliyofanyika juzi katika Kanisa la Kristo Mfalme Madaba, wilayani hapa.

Askofu Chiteto alipatwa na umauti muda mfupi baada ya kuhubiri katika misa ya kifo cha Hilda Lugendo aliyekuwa mke wa askofu mwenzake.

Akisimulia jinsi Chiteto alivyopata uaskofu, Dk Mndolwa alisema hakuwania nafasi hiyo, lakini walijikuta wakifanya uamuzi wa kumuingiza kwenye mchakato siku sita kabla ya kifo chake.

Alisema hata nafasi ya kutoa mahubiri ya kuuaga mwili wa Hilda alipangiwa Askofu Sospeter Ndenza wa Dayosisi ya Kibondo iliyoko Mkoa wa Kigoma, lakini alipochelewa kufika, wakaamua kumpatia nafasi hiyo Askofu Chiteto ambaye mahubiri yake, anasema yalikuwa kama anawaaga waamini na viongozi wenzake wa kanisa hilo.

“Mahubiri aliyoyatoa yalikuwa ya maajabu, kwa sababu ilikuwa ni hotuba ya maandalizi ya kuaga, jambo la msingi ni kila mmoja kujiweka tayari,” alisema Askofu Mndolwa.

Alisema maajabu mengine, ni kawaida baada ya mahubiri, mhubiri ilikuwa aende kumpatia mkono lakini alijikuta akiimbisha wimbo 313.

“Kwa hivyo sikuwahi hata kumpa mkono, kifo kilinitangulia...ni mipango ya Mungu” alisema Askofu Mndolwa .

Askofu mstaafu wa kanisa hilo Dayosisi ya Tanga, Dk Philip Baji ambaye pia ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha St John jijini Dodoma alisema Àskofu Chiteto amekufa akiwa hajahamisha vyombo vyake chuoni hapo.

“Chiteto alikuwa mwanafunzi wangu chuo cha St John na baadaye akajakuwa mwalimu hapohapo chuoni. Alisimikwa na kuwekwa wakfu 28/8/2022 kuwa Askofu wa Dayosisi ya Mpwapw. Hata vyombo vyake chuoni alikuwa hajahamisha” alisema Askofu Baji.

Alisema Askofu Chiteto amefariki akiwa hajaendesha hata ibada moja, lakini alikuwa mWinjilisti hodari aliyebobea katika mahubiri.

Mwili wake ulisafirishwa kupelekwa Dodoma katika Chuo cha St John na baadaye kupelekwa Mpwapwa kwa ajili ya maziko leo Jumatano.