Asakwa akidaiwa kutupa kichanga chooni

Muktasari:

  • Jeshi la Polisi mkoani Singida, linawatafuta watuhumiwa wawili kwa kosa la kumtupa mtoto wa siku moja chooni.

Singida. Jeshi la Polisi mkoani Singida, linawatafuta watuhumiwa wawili kwa kosa la kumtupa mtoto wa siku moja chooni.

Akizungmuza na Mwananchi Digital leo Julai 18, 2023, Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Singida, ACP Stella Mutabihirwa, amesema wanaendelea kuwatafuta watuhumiwa hao kwa kosa la kumtupa mtoto wa siku moja chooni.

“Mtuhumiwa wa kwanza ni hafahamiki kwa jina wala anwani ya makazi yake, huyu anadaiwa kutenda kosa la kumtupa mtoto wake wa kike mwenye umri wa siku moja huko katika kijiji cha Ikungi, hata hivyo, mtuhumiwa wa pili ni Mwanaidi Sudi (51),” amesema.

Kwa mujibu wa Kamanda huyo, Balozi wa nyumba 10 (hajatajwa jina lake) ndiye aligundua kutupwa kwa mtoto huyo mchanga, katika shimo la choo.

Kamanda Stella amesema mtoto huyo amefikishwa katika Hospitali ya Rufaa Mandewa mjini Singida, na hali yake inaendelea vizuri.

“Jeshi la Polisi linaendelea na uchuguzi juu ya tukio hilo ambapo tunashirikiana na raia wema, msako mkali unaendelea kuhakikisha muhumiwa anakamatwa na kufikishwa mahakamani,” amesema Kamanda Mutabihirwa.