Asasi za kiraia nchini zaiomba serikali kutunga sheria ya kudhibiti ukatili

Muktasari:

Asasi za kiraia nchini zimeiomba Serikali kuchukulia matukio ya ukatili dhidi ya mwenza yanayoendelea hivi sasa, kama jambo la dharura na kuitungia sheria ya ukatili majumbani ili kukomesha matukio hayo yanayoongezeka katika jamii nchini.


Arusha. Asasi za kiraia nchini zimeiomba Serikali kuchukulia matukio ya ukatili dhidi ya mwenza yanayoendelea hivi sasa, kama jambo la dharura na kuitungia sheria ya ukatili majumbani ili kukomesha matukio hayo yanayoongezeka katika jamii nchini.

Akizungumza jana Oktoba 27 jijini Arusha wakati wa mjadala wa mada ya ukatili dhidi ya mwenza, uliohusisha wadau wa asasi za kiraia, viongozi wa dini, serikali na wahanga wa matukio hayo, Mkurugenzi wa Sera, Uchechemuzi na Maboresho wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) Fulgence Masawe amesema wamekutana kutafuta ufumbuzi wa matukio hayo kwani jambo hilo  limekuwa ni janga la kitaifa  hivi sasa.

Amesema kuwa, wameona kuna umuhimu wa kukabiliana na matukio hayo na kushauri serikali namna bora ya kukomesha matukio hayo ambayo kila kukicha yanazalisha walemavu na vifo.

"Katika wiki hii ya asasi za kiraia tumeweka mada hii ili tuje na mpango mkakati wa kushauri serikali jinsi ya kukabiliana na haya na tunaomba itungwe  sheria ya ukatili majumbani na kwa dharura sababu wengi wanaokumbwa na matukio haya ni wenza na yanafanyika kwenye nyumba zetu," amesema.

Fulgence amesema  kuwa, ni hatari kwa ongezeko la matukio ya kukatana mikono, mauaji na kuumizana maeneo mengine ya mwili kwa Tanzania kwani yakiachwa yaendelee yataharibu kizazi kijacho.

Aidha amesema kuwa sababu kubwa ya ongezeko la matukio hayo ni wivu wa kimapenzi,ukatili wa kiuchumi na matatizo ya afya ya akili.

Naye Mtafiti Mwandamizi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Fundikila Wazambi akiwasilisha ripoti ya ukatili dhidi ya mwenza amesema kwa mujibu wa takwimu za  dunia inaonyesha kati ya wanawake watatu mmoja wao amefanyiwa ukatili wa kimwili au kingono.

Amesema kuwa, ukatili huo hufanywa na wenza wao ambao ni mume, mke au rafiki wa kiume au wa kike kwenye nyumba zao.

"Inaonekana nyumbani kwa sasa ni sehemu hatari kwa wakina mama sababu ya  mauaji na hata kusababishiwa ulemavu  hali hii lazima wadau tuungane kutafuta mbinu za kukomesha matukio haya maana tusipiga kelele sisi wenyewe hakuna atakayekuja kutetea  jamii yetu,” amesema.

Kwa upande wake mmoja wa wahanga wa ukatili wa mwenza,Veronika Kidemi ambaye ni Mwalimu wa Shule ya Sekondari Kiranyi wilayani Arumeru amesema yeye alikatwa na mume wake, kiganja cha mkono wa kulia na sime Septemba 26 mwaka 2020 nyumbani kwake Kijiji cha Siwandeti.

"Sababu kubwa wivu wa mapenzi yeye mume wangu Alfanyo Ombeni, siku ya tukio alirudi Arusha kimyakimya na alipofika nyumbani hakunikuta, mimi nilienda kununua mahitaji ya ndani ili kujikimu na watoto wangu wawili, nilipofika nyumbani alianza kunirushia matusi na akachukua sime na kunitenganisha kiganja changu, ilikuwa ngumu ila nashukuru sasa nimezoea hali hii kwa msaada na ushauri niliopewa na wadau mbalimbali na maisha yanaendelea," amesema.

Ameongeza kuwa, kabla ya kukatwa kiganja chake, mwanzoni mwa ndoa yao ilikuwa ya karaha sababu ya  matusi na vipigo, lakini ndugu walimsihi kuvumilia kwa kuwa ana watoto, hadi alipopata ulemavu huo na kila mmoja kuona kumbe alikuwa na mwanaume katili.