Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Asimulia alivyojifungulia barabarani

Muktasari:

  • Amejifungulia njiani wakati akitafuta usafiri wa kumpeleka kituo cha afya.

Dar es Salaam. Mkazi wa mtaa wa Kipera, Kata ya Kitunda wilayani Ilala, jijini Dar es Salaam, Mariam Jeremia amejifungulia njiani wakati akitafuta usafiri wa kumfikisha kituo cha afya.

Mariam (25), amesema kwa msaada wa muuza duka la dawa, alijifungua mtoto wa kike akiwa amelala mchangani.

Tukio hilo limetokea Februari 29, 2024 saa tatu usiku, Mariam aliposhikwa uchungu wa kujifungua.

Kwa msaada wa majirani zake wawili aliongozana nao kutoka nyumbani kwa miguu kuelekea barabarani ambako wangepata usafiri wa kwenda Kituo cha Afya cha Buza.

Akizungumza na Mwananchi Digital nyumbani kwake leo Jumapili, Machi 3, 2024, Mariam amesema alipojihisi uchungu alimshirikisha jirani yake aliyemwambia aite usafiri wa kumpeleka kituo cha afya.

"Kutokana na ubovu wa barabara za huku niliamua kuita gari, wakati huo majirani zangu wakiniambia nijikaze ili nisogee sehemu ambayo tutalikuta gari, niliwakatalia nikiwaambia siwezi kutembea," amesema Mariam.

Baada ya kukataa, amesema walimshika mmoja kulia na mwingine kushoto wakimsaidia aweze kutembea, ili kufika barabarani kwa ajili ya kupanda gari.

Kutoka ilipo nyumba yao hadi barabarani kuna umbali karibu nusu kilomita na wakati wanatembea, amesema walikuwa wakiendelea kuwasiliana na dereva wa gari.

Wakiwa njiani, amesema alipokea simu kutoka kwa dereva akimweleza amezuiwa kupita na wafanyakazi wanaohusika na ujenzi wa barabara ya Mtaa wa Kapera, licha ya kuwaeleza anafuata mgonjwa.


Kipande cha barabara hiyo kinachoelezwa huwa na utelezi wakati wa mvua kinafanyiwa matengenezo kwa kuwekwa zege.

Mariam amesema wakati uchungu ukiendelea, majirani zake hawakujua namna ya kumsaidia, zaidi ya kumwambia wampandishe kwenye bodaboda kitendo ambacho kwa upande wake amesema asingeweza,  kwani alihisi anakaribia kujifungua.

"Baada ya kuona nashindwa kila kitu niliwaomba wanitandikie kitu chini, nafikiri kwa sababu ya uoga hawakufanya hivyo, matokeo yake mtoto alitoka na kuanguka kwenye michanga, hawakujua cha kufanya," amesema.

Amesema wakati wanashangaa alitokea mwanamke aliyemsaidia kukata kitovu na alimchoma sindano kukata damu iliyokuwa ikimtoka.

Hata hivyo, damu iliendelea hadi alipopelekwa kituo cha afya.

Baadaye ilibainika mwanamke aliyemsaidia ni mhudumu katika duka la dawa lililopo jirani na alikojifungulia.

Amesema hayo yote yalitokea yakishuhudiwa na watu waliokuwepo eneo hilo, wakiwemo wanaume, ambao walisimama wakimuangalia wasijue cha kufanya.

Wakati hayo yakiendelea, amesema dereva wa gari baada ya kukataliwa kupita aliamua kuchukua bodaboda kumfuata na akamkuta njiani akiwa ameshajifungua.

"Dereva alivyoona natokwa damu, aliniambia Mariam ngoja nikaombe tena, ili tukupeleke hospitali tunaweza kukupoteza wewe na mtoto kwa sababu damu zinaendelea kutoka," amesema.

Amesema dereva alipokwenda akaruhusiwa kupita ndipo alipoweza kumfikisha Kituo cha afya Buza.


Kauli ya aliyemsaidia

Muuzaji wa duka la dawa, Magreth Ndunguru (50), akizungumza na Mwananchi Digital amesema alipofika eneo la tukio alikuta Mariam ameshajifungua.

Kitu cha kwanza alichofanya anasema alimchukua mtoto kutoka kwenye mchanga na kuanza kumfuta na kisha kumkata kitovu.

Amesema alikuta kondo likiwa limeshatoka kwa mama, hivyo aliwakusanyia vitu vyao vyote na kuwakabidhi, akiwa amemchoma sindano kuzuia damu isiendelee kutoka.

"Nilikuta mtoto yupo kwenye mchanga nikamchukua, nikamfuta michanga nikakata kitovu, nikamfunika na nguo, nilimchoma sindano ya kuzuia damu isiendelee kutoka," amesema.

Alichoambiwa kituoni

Mariam amesema alipofika Kituo cha afya Buza aliulizwa imekuwaje amechelewa hadi akajifungulia njiani, kitendo kilichosababisha kutokwa na damu nyingi na kukosa huduma ya kwanza.

Amesema aliwaeleza yote, pia aliwapa taarifa kuwa alichomwa sindano ya kuzuia damu isiendelee kutoka.

"Pale hospitali walivyoona vile walinisema kwa nini nilichelewa, lakini dereva alinisaidia kunitetea kuwa alizuiliwa kupita hadi kufikia hali hiyo," amesema.

Amesema alikaa katika kituo hicho hadi aliporuhusiwa kurejea nyumbani Machi mosi, 2024 saa 10.00 jioni akiwa amepewa huduma zote.

Amesema kwa sasa wanaendelea vizuri yeye na mtoto wake, lakini anaona mwanawe amevimba jicho moja, hivyo leo atampeleka tena kituo cha afya.

Mashuhuda wanena

Dereva wa bodaboda, Athuman Omary 'Kimbingu' mkazi wa Mtaa wa Kipera, amesema kwa mara ya kwanza ameshuhudia mwanamke akijifungua, kitendo ambacho anasema si sawa.

Amesema hawakatai maendeleo ya matengenezo ya barabara, lakini kitendo cha kufunga njia pande zote hakina maana.

"Hatukatai wanajenga, lakini wangeacha upande mmoja ili kuwezesha magari na bodaboda kupita kama huyo mama aliyejifungua njiani wangeruhusu apite, hali hiyo isingetokea," amesema.

Amesema kuna njia mbadala ambazo bodaboda wameelekezwa kupita wakati matengenezo ya kipande cha barabara yakiendelea, lakini wenye makazi jirani wameamua kuweka magogo ili wasipite.

Fatma Masongela, mkazi wa Kipera amesema kilichotokea ni udhalilishaji kwa mwanamke kwa kuangaliwa na watu alivyokuwa anajifungua, hivyo kutweza utu wake.

"Endapo angewahi hospitali yote hayo yasingetokea, kwa hiyo wao wamethamini barabara kuliko uhai wa mtu. Ingekuaje angefariki mama au mtoto au wote kwa pamoja, wangekubali kufungulia maiti ipitishwe kuliko mtu kuwa mzima?" amehoji Fatuma.

Serikali ya Mtaa

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kipera, Hussein Yusuph amesema taarifa ya mkazi wake kujifungulia njiani anazo.

Hata hivyo, amedai muda wake wa kujifungua ulikuwa umefika, lakini si kizuizi cha barabara kilichosababisha ajifungulie njiani.

"Mume wake alizembea kumpeleka hospitali mapema, sasa alipomtoa nyumbani kwake kumleta kwenye kizuizi wakati anaendelea kufanya utaratibu afunguliwe, yule binti akajifungua karibu na dukani, lakini baadaye likachukuliwa gari akapelekwa hospitali," amesema Yusuph.

Amesema kumekuwa na malalamiko kuhusu ubovu wa barabara na kusababisha ajali kwa magari kuanguka kutokana na utelezi katika eneo la milima, hivyo walichukua hatua ya kwenda sehemu husika kuomba fedha za kukarabati eneo hilo.

Kuhusu kufunguliwa barabara hiyo, amesema hadi jana barabara hiyo ya zege inatimiza siku ya 11 na kutokana na maelekezo ya mkandarasi wataruhusu magari na bodaboda kupita baada ya siku 21 kwa sababu ya kuendelea kutengemaa zaidi.

"Barabara hii ya zege ikiwa na siku saba tulisharuhusu magari ya wagonjwa wa dharura kupita akiwepo huyo mama aliyejifungua na tunaliwasiliana na mkandarasi kuhusu hilo, alitupa ruhusa ya kupitisha magari madogo ya wagonjwa," amesema.

Charles Mwalongo, mhandisi wa barabara amesema ili magari yaruhusiwe kupita kwenye barabara iliyowekwa zege inatakiwa zipite siku 21.

Hata hivyo, amesema endapo zege itakuwa imechanganywa vizuri na kutumika kwa malighafi bora, inaweza kukaa siku saba hadi 14 na ikatokea dharura inaweza kutumika ndani ya siku nne.

"Uimara wa barabara unategemea mchanganyo wake maana zipo zinazoweza kutumika ndani ya siku nne, lakini kuanzia siku saba hadi 14 zege linakuwa limekauka, lakini kiwango bora na imara kwa barabara kutumika ni siku 21," amesema.