Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Uchungu wa kujifungulia njiani, wanawake wachangishana

Baadhi ya wanawake kijiji cha Bukore wilayani Serengeti, wakiwaonyesha wanahabari nyumba ya kuishi mganga wa zahanati ya Bukore, ambayo wanaijenga kwa kuchangishana fedha kidogo kidogo kuanzia Sh2,000. Katikati ni mwanzilishi wa wazo hilo, Robina Thomas.Picha na Daniel Mjema

Muktasari:

  • Waamua kujenga nyumba ya mganga wakichangishana kati ya Sh2,000 hadi 10,000

Serengeti. Kinamama 135 wa kijiji cha Bukore katika Wilaya ya Serengeti mkoani Mara, wamejitolea kujenga nyumba ya kuishi mganga wa zahanati mpya, ambapo kila mmoja alichanga kati ya Sh2,000 na Sh10,000 hadi zikawezesha ujenzi kuanza.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu, Januari 8, 2024 waliotembelea eneo la mradi huo, Katibu wa waasisi wa kikundi cha ujenzi wa nyumba ya mganga, Robina Thomas, alisema waliamua kufanya hivyo ili kurahisisha huduma za kiafya kijijini hapo.

“Baada ya maombi ya wanakijiji, TANAPA (Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania) walikubali kutujengea zahanati, lakini bila jengo la daktari,”ameeleza.

Mradi huo wa Zahanati hiyo ya kisasa unatekelezwa na Tanapa, kupitia mradi mradi wa uhifadhi na maendeleo (SEDCP) chini ya ufadhili wa benki ya Ujerumani (kfw) na unatarajiwa kuanza kutoa huduma kwa wananchi Aprili 2024.

“Kwa kuwa sisi wanawake na watoto ndio tunaopata shida zaidi, tukafikiri ni vyema daktari apate pa kuishi hapa hapa karibu,” amesema Robina.

Kwa mujibu wa Robina, alisema yeye na viongozi wengine wakaanza kuhamasisha wanawake wa Bukore na kuwaeleza umuhimu wa kuwapo daktari anayeishi karibu na zahanati hiyo hasa pale kunapojitokeza uhitaji wa dharura.

Juhudi za kina mama hao ziliwawezesha kununua matofali, mifuko 100 ya saruji na fedha za mafundi huku wakichangia nguvu katika kupeleka mawe na mchanga.

“Tumeshaliinua jengo ingawa kwa sasa tumesimama. Tulikubaliana kwanza tuwapeleke shule watoto ndio turejee kwenye michango,” amesema.

Mjumbe wa kikundi hicho cha mfano katika ushiriki wa wananchi katika maendeleo, Mwenoki Magambo, amesema mkutano wao wa kwanza ulifanyika chini ya mti eneo la ujenzi, kina mama walichangishana Sh5,000 kila mmoja.

“Hatukuishia hapo. Tukachangishana tena Sh2,000 kwa kila mwanamke halafu awamu nyingine tukachanga Sh10,000 kila mtu,” amesema Magambo.

Mwenoki, ambaye ni mmoja wa waathirika wa kutokuwapo kwa huduma za afya kijijini hapo, amesema awali walilazimika kwenda kijiji jirani au mjini Mugumu kufuata huduma na kulikuwa na matukio ya baadhi yao kujifungulia njiani.

“Mimi nilijifungulia njiani mtoto wangu wa pili. Niliikuwa ninapelekwa hospitali mjini (Mugumu), lakini Mungu ni mwema, wakanipokea na kunihudumia,”amesema Magambo.

“Ni kutokana na kumbukumbu hizo ndio maana nimekuwa mstari wa mbele katika ujenzi wa nyumba ya mganga ili kuunga mkono juhudi za Tanapa kusaidia wananchi. Tanapa Mungu aendelee kuwalinda katika shughuli zao,” amesema.

Ofisa Mhifadhi wa Hifadhi ya Taifa Serengeti anayeshughulikia Uhusiano wa Umma, Idara ya Ujirani Mwema, Robert Masobeji, amesema ujenzi wa zahanati hiyo ni moja kati ya miradi 35 inayotekelezwa na Tanapa katika wilaya ya Serengeti.

“Mradi huu ni ni sehemu ya miradi ya ushirikishaji wananchi manufaa ya uhifadhi. Katika wilaya ya Serengeti pekee ipo miradi 35. Hii imefanya wananchi wajue umuhimu na kuthamini uhifadhi. Hii inawafanya wawe mabalozi wetu,” amesema.

Masobeji amesema miradi hiyo ni ya afya, elimu na barabara huku akifafanua vigezo vya kupeleka miradi katika vijiji vinavyozunguka hifadhi kuwa ni pamoja na ushiriki wa wananchi kupunguza uhalifu dhidi ya wanyama pori ikiwamo ujangili.

“Vijiji vilivyopunguza uhalifu hasa ujangili ndivyo vinavyonufaika na miradi yetu,” amesema Masobeji na kueleza kuwa hii imewapa hamasa wananchi ya kuwafichua wale wanaojiandaa kufanya ujangili au wanaoingia hifadhini kufanya ujangili.