Askari 34,106 nchini Tanzania wapandishwa vyeo

Friday June 11 2021
vyeo pic

Waziri wa mambo ya ndani,George Simabachawene akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma leo Juni 11,2021 kuhusu upandishwaji vyeo maafisa,wakaguzi na askari wa jeshi la polisi,magereza,uhamiaji na zimamoto na uokoaji.Picha na Jonathan Musa

By Bakari Kiango
By Jonathan Musa

Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Ndani nchini Tanzania, George Simbachawene amewapandisha vyeo maofisa, wakaguzi na askari 34,106 wa Jeshi la Polisi, Magereza, Zimamoto na Idara ya Uhamiaji.

 Simbachawene ameeleza hayo leo Ijumaa Juni 11, 2021 wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma na kubainisha kuwa hatua hiyo ni utekelezaji wa agizo wa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

 Katika maelezo yake, Simbachewene amesema askari 34,106 ni wale wanaostahili kupandishwa vyeo katika kipindi cha mwaka wa fedha 2018/19, 2019/20 na 2020/21 na kwamba  askari 26,464 wa jeshi la polisi wamepandishwa vyeo.

 “Kati yao warakibu waandamizi wa polisi 110 wamepandishwa cheo cha makamishna wasaidizi. Warakibu wa polisi 110 wamepandishwa cheo cha warakibu waandamizi wa polisi.”

“Warakibu wasaidizi wa polisi 241 wamepandishwa cheo kuwa warakibu wa polisi. Wakaguzi wa polisi 745 wamepandishwa cheo cha warakibu wasaidizi wa polisi huku wakaguzi wasaidizi 890 wamepandishwa cheo cha wakaguzi wa polisi,” amesema Simbachawene.

 Kwa mujibu wa Simbachawene jumla ya askari  R & F 4,148 wamepandishwa vyeo kuwa wakaguzi wasaidizi wa polisi. Pia askari R & F 20,220 wamepandishwa vyeo mbalimbali kutoka polisi konstebo kwenda koplo 13,751, na kutoka koplo kwenda sajini 5,619.

Advertisement

Waziri Simbachewene amesema kutoka sajini kwenda stafu sajini ni 800 na kutoka sajini kwenda meja ni askari 50  huku Jeshi la Magereza likiwapandisha vyeo jumla ya maofisa wakaguzi na askari 6,310.

Amesema kati ya hao warakibu waandamizi wa Magereza saba wamepandishwa cheo kuwa makamishna wasaidizi wa magereza na warakibu wa Magereza 14 wamepandishwa cheo kuwa warakibu waandamizi wa Magereza.

Kwa upande wa Zimamoto na Uokoaji, Simbachawene amesema jumla maofisa wakaguzi na askari 149 wamepandishwa vyeo na katika Idara ya Uhamiaji askari 1,183 wamepandishwa vyeo vya ngazi mbalimbali.


Advertisement