Askari Magereza atuhumiwa kubaka, kulawiti

Muktasari:
- Jeshi la Polisi Mkoa wa Ilala linamshikilia Askari Magereza Said Hassan (26) mkazi wa Ukonga jijini Dar es Salaam kwa tuhuma za kumbaka na kumlawiti msichana awenye umri wa miaka (29) jina lake limehifadhiwa.
Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Mkoa wa Ilala linamshikilia Askari Magereza Said Hassan (26) mkazi wa Ukonga jijini Dar es Salaam kwa tuhuma za kumbaka na kumlawiti msichana (29) jina lake limehifadhiwa.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Ijumaa Septemba 3, 2021, Kamanda wa Polisi mkoa huo, ACP Debora Magiligimba amesema Septemba Mosi, 2021 saa 5:30 usiku kwenye Barabara ya Madafu Ukonga mtuhumiwa huyo ambaye ni Askari Magereza mwenye namba B9780 akiwa na mwenzake ambaye hajakamatwa, inadaiwa walimkamata kwa nguvu binti huyo na kumuingiza kwenye gari dogo kisha kuondoka naye.
Magiligimba amesema watuhumiwa hao waliondoka na binti huyo hadi kwenye nyumba moja iliyopo karibu na Kambi ya KMKM Ukonga Magereza na kuanza kumbaka na kumlawiti kwa zamu.
"Baada ya kumaliza kumbaka na kumlawiti watuhumiwa hao waliendelea kumfanyia binti huyo vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa kumuingiza mkono katika sehemu zake za siri na kumsababishia majeraha na maumivu makali," amesema.
Kamanda Magiligimba amesema baada ya mtuhumiwa huyo kugundua anatafutwa na polisi kutokana na tukio hilo, Septemba 2, 2021 alijaribu kujiua kwa kujinyonga kwa kamba ya manira na kuacha ujumbe uliosomeka "Nisamehe bure kwa uamuzi wangu niliouchukua kwani tukio nililolifanya nitaonekana nimekufa kizembe."
Kamanda amesema ujumbe huo ulikuwa unawalenga mkuu wake wa kazi pamoja na askari wenzake ambao alikuwa anafanya nao kazi, lakini kabla ya kufanikisha azma hiyo ya kujiua, alikamatwa na kufikishwa katika kituo cha polisi.
Aidha kamanda amesema jeshi hilo linaendelea kumtafuta mtuhumiwa mwenzake ambaye alikimbia baada ya tukio hilo na kumtaka ajisalimishe kituo chochote cha polisi.
"Nitoe wito kwa wananchi wa Mkoa wa Kipolisi Ilala kuacha kufanya vitendo hivi vya kikatili kwa wanawake. Niwaombe pia wananchi waendelee kutoa taarifa dhidi ya matukio haya yanayosababisha wanawake kuathiriwa kimwili na kisaikolojia, " amesema.