Askari waliopambana na Hamza watunukiwa hati ya ujasiri

Monday September 20 2021
Askari pc
By Waandishi Wetu

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi limewatunuku hati ya ujasiri askari waliopambana katika tukio la mtu aliyefahamika kwa jina la Hamza Mohamed, kuwashambulia askari na kuwaua wanne katika makutano ya barabara ya Ali Hassan Mwinyi.

Tukio hilo lilitokea Agosti 25 mwaka huu ambapo Hamza aliwaua askari watatu na mlinzi wa kampuni ya SGA kabla ya yeye kuuliwa.

Askari waliopewa hati za ujasiri ni Adam Malya, Mashaka Magaji, Manfred Mrope, Majige Chuma, Faraji Hemed na Albano Mwalunda.

Wengine ni Juma Chacha, John Alex, Issa Godwin, Halifa Mrutu na Selenga Nyagawa.

Soma hapa:Huyu hapa Hamza

Akizungumza mara baada ya kuwatunuku askari hao leo Septemba 20 kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la polisi nchini, Simon Sirro, Kamanda Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema lilikuwa tukio kubwa ambalo kama lisingedhibitiwa haraka lingeweza kuleta madhara makubwa.

Advertisement

Amesema katika tukio hilo kulikuwa na askari wengi na wote walifanya kazi nzuri lakini hao 11 walifanya vizuri zaidi.

“Leo ni miongoni mwa siku muhimu wa jeshi la polisi katika kuendelea kutekeleza majukumu yake, wote tunakumbuka tukio lililotokea Agosti 25, askari hawa walipambana kuhakikisha madhara makubwa hayatokei ambapo kwa mamlaka ya kisheria ya jeshi la polisi IGP Sirro amewapa zawadi ya hati za ujasiri na fedha kwa kadri alivyoona inafaa.

“Tukumbuke kazi ya askari polisi ni miongoni mwa kazi ngumu tofauti na watu wanavyoitazama. Jukumu walilopewa ni kubwa la kupita kiasi la kuwalinda wananchi pamoja na mali zao.

“Mmeshuhudia wakipoteza maisha si hali ya kawaida, ukaamua kufa kwaajili ya watu wengine si kazi ya kubeza, si kazi ya kuitafsiri kirahisi rahisi kama watu wanavyofanya,” amesema Muliro.

Soma hapa:Ndugu wa Hamza washangazwa na uchunguzi wa Polisi

Amebainisha kuwa hawatatoa nafasi kwa muhalifu ambaye hajitaki, na kilichofanyika Agosti 25 ni chachu ya jeshi hilo kuendeleza mapambano dhidi ya uhalifu.

Hata hivyo, Kamanda Muliro amesema jeshi hilo litatoa zawadi ya sh2 milioni kwa atakayetoa taarifa za majambazi au wanaofanya uhalifu kwa kutumia silaha, ambazo zitafanikisha kuwakamata wao pamoja na silaha hizo.

Imeandikwa na Tatu Mohamed na Rhoda Kivugo

Advertisement