Ndugu wa Hamza washangazwa na uchunguzi wa Polisi

Muktasari:

  • Familia ya Hamza Mohamed aliyewapiga risasi na kuwauwa askari watatu, mlinzi mmoja wa kampuni binafsi na kisha naye kuuawa kwa kupigwa risasi, wameeleza kusikitishwa na taarifa kutoka polisi kuwa ndugu yao alikuwa gaidi.


Dar es Salaam. Familia ya Hamza Mohamed aliyewapiga risasi na kuwauwa askari watatu, mlinzi mmoja wa kampuni binafsi na kisha naye kuuawa kwa kupigwa risasi, wameeleza kusikitishwa na taarifa kutoka polisi kuwa ndugu yao alikuwa gaidi.

Akizungumzia uchunguzi wa polisi, jana Alhamisi, Setemba2, 2021 msemaji wa familia ya Hamza, Abdulrahman Hassan amesema wamekuwa wakimuona marehemu akiwa mtu wa kawaida ambaye hakuwa na tabia yoyote ya kigaidi.

‘‘Dah! Sisi tulikuwa tukimuona Hamza kama mtu wa kawaida asiye na mwenendo wa kigaidi, amesema kwa mshtuko.

Kuhusu Hamza kujifunza ugaidi kupitia mitandao, amesema: “Dada….! Hamza anajulikana, watu wamemzungumzia wanavyomfahamu, sisi hatuna cha kuongeza kama polisi wanadai hivyo.’’

Alipoulizwa kama familia inafahamu lolote kuhusiana na viashiria vya ugaidi vinavyodaiwa kuwa Hamza alikuwa navyo, Hassan amesisitiza walikuwa wakimuona Hamza ni mtu wa kawaida na si mwenye nyendo za kigaidi.

Kuhusu Hamza kuishi kisiri huku akiwa amegubikwa na viashiria vyote vya ugaidi na kujifunza mambo mbalimbali kupitia mitandao ya kijamii, hasa ile ambayo inaonyesha matendo ya Al-Shabab na makundi kama ya ISIS, msemaji huyo amesema hawezi kuzungumzia chochote juu ya jambo hilo

Maelezo hayo ya Hassan yametokana na taarifa ya polisi iliyotolewa jana na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Camillius Wambura ambaye amesema kwamba uchunguzi wa awali umebaini kuwa Hamza alikuwa gaidi wa kujitoa mhanga.

DCI asema uchunguzi wao umebaini Hamza alikuwa gaidi

Hamza aliuawa kwa kupigwa risasi Agosti 25 baada ya kuwaua askari polisi watatu na mlinzi mmoja karibu na Ubalozi wa Ufaransa jijini Dar es Salaam.

Jana akiwa jijini Mwanza jana, DCI Wambura amesema kuwa uchunguzi wao ulilenga kujua utambulisho wa Hamza, ni nini kilimpa msukumo wa kuua na washirika wake ni akina nani.

DCI Wambura amesema katika uchunguzi huo, polisi waligundua kwamba Hamza aliishi maisha ya kibinafsi sana na viashiria vyote vya ugaidi.

Sirro: Njooni mchukue mwili wa Hamza

“Kwa muda mrefu, alikuwa akijifunza kupitia mtandao kuhusu shughuli za ugaidi wa Al-Shabab na ISIS,” amesema Wambura.

Amesema Hamza pia alikuwa na mawasiliano ya moja kwa moja na watu wanaoishi katika nchi ambazo zinakabiliwa na matukio ya ugaidi hivyo kumfanya awe na msimamo mkali.