Huyu hapa Hamza

Wafanyakazi wa Hamza mgodini wamzungumzia

Muktasari:

  • Swali kuu juzi lilikuwa ni nani aliyetekeleza mauaji haya ya polisi. Baada ya kufahamika kuwa ni Hamza Mohammed (pichani), watu mbalimbali wanaomfahamu tangu utoto, Dar es Salaam na Chunya, wamemwelezea kwa namna tofauti.

Dar es Salaam. Swali kuu juzi lilikuwa ni nani aliyetekeleza mauaji haya ya polisi. Baada ya kufahamika kuwa ni Hamza Mohammed (pichani), watu mbalimbali wanaomfahamu tangu utoto, Dar es Salaam na Chunya, wamemwelezea kwa namna tofauti.

Huyu ndiye anatajwa kuhusika na shambulio la risasi katika makutano ya Barabara ya Kinondoni na Kenyatta Drive lililosababisha vifo vya askari wanne, watatu wa polisi na mmoja wa kampuni binafsi.

Katika shambulio hilo lililotokea juzi mchana, Hamza aliua askari hao, akiwamo mlinzi mmoja wa Kampuni ya SGA, kabla ya yeye kuuawa katika mapambano hayo.

Shambulio hilo lililotokea nje ya Ubalozi wa Ufaransa lilizua hofu kwa wakazi mbalimbali wa jiji la Dar es Salaam.

Katika tukio hilo pia, watu wengine sita walijeruhiwa, wakiwamo polisi.

Hamza aliyekuwa akiishi Mtaa wa Fire uliopo Upanga, Dar es Salaam, majirani zake walisema jana kuwa muda mwingi alikuwa haonekani mtaani hapo kutokana na kuendesha shughuli zake mikoani.

Jirani ambaye hakutaka kutaja jina lake, alimwelezea Hamza kwa mazingira aliyoishi na wazazi wake kabla na baada ya kuwapoteza baba mzazi na dada yake.

Alisema Hamza anayekadiriwa kuwa na miaka 30, alizaliwa mtoto wa tatu kwenye familia ya watoto saba, wakiwamo wanaume watatu.

“Hamza ninavyomfahamu, ni kijana mpole, tangu nimehamia hapa mwaka 2001 sijawahi kusikia baya kuhusu yeye, sio kijana wa kuishi vijiweni, ni mtu anayefanya mambo yake na hajawahi kugombana na jirani yeyote,” alisema.

Pia, Hamza alikuwa mteja wake wa muda mrefu katika duka lake lililopo jirani na nyumbani kwao na wakati alinunua vitu na kuondoka kwa kuwa hakuwa mwongeaji.

“Si mtu anayeonekana sana mtaani, unaweza kukaa hata wiki tatu bila kumuona,” alisema.

Mfanyabiashara mwenye duka lililopo karibu na nyumba aliyokuwa akiishi Hamza, alisema kijana huyo alikuwa mteja wake asubuhi, “kila alipokuwa nyumbani alikuja kununua mkate hapa, ni mpole na mtulivu.”

Kauli hiyo, haikutofautiana na jirani mwingine ambaye pia hakutaka kutaja jina lake, akisema Hamza alikuwa mpole tangu utotoni, mcha Mungu na mwenye heshima.

Alisema japokuwa ni jirani yake lakini kuna wakati walikuwa wakikaa hadi siku tatu bila kuonana kwa sababu kila mmoja alikuwa akikaa ndani kwake.

“Si yeye tu, hata mama yake tulikuwa tunaweza kukaa siku tatu hatujaonana, lakini huyu kijana muda mwingi aliutumia huko Mbeya katika shughuli zake,” alisema.

Mmoja wa madereva Taxi wanaoegesha magari jirani na nyumbani kwao, alisema alikuwa akimfahamu kijana huyo na mbali na kusali, pia alikuwa mtu aliyependa starehe.

“Ilikuwa ikifika muda wa swala, anakwenda msikitini lakini starehe pia alizipenda na alijua kutumia pesa zake,” alisema dereva huyo.

Vipi kuhusu umiliki mgodi?

Jirani alisema kuhusu umiliki wa migodi wilayani Chunya Mkoa wa Songwe, familia hiyo ilirithi kutoka kwa baba yao aliyefariki dunia siku za nyuma.

“Hata hapa alikuwa hakai sana, alikuwa anakuja kumuangalia mama yake na kuondoka kurudi Chunya na wakati mwingine alikuwa akimpeleka hospitalini kwa sababu anasumbuliwa na magonjwa ya utu uzima,” alisema.

Alisema Hamza alikuwa akipenda kutumia pikipiki na hata siku ya tukio asubuhi alitoka na pikipiki yake kabla ya kuirudisha na kuondoka tena hadi taarifa za tukio liliposikika.


Serikali ya Mtaa

Mwenyekiti wa Mtaa wa Fire, Joha Lemki alisema Hamza ni mkazi wa eneo hilo kwa muda mrefu.

Hata hivyo, hakutaka kuzungumzia kwa kina suala hilo kwa kile alichoeleza lipo kwenye vyombo vya dola kwa uchunguzi.

“Kwa kuwa jambo liko mikononi mwa polisi, wao ndio wanaweza kulizungumzia. Mimi pia nina wakubwa zangu, nimewaachia hilo jukumu,” alisema Lemki.

“Ni kweli alikuwa raia kama raia wengine, ni mkazi wa mtaa wangu. Hilo nakubaliana kabisa, wameishi pale muda mrefu tu.”

Kijana mwingine alisema Hamza alikuwa akipendelea zaidi magari na pikipiki.

“Alikuwa ni mshikaji akikutuma lazima akuachie chochote kitu au akikupa kazi labda ya kufanya usafi anakutoa kiroho safi,” alisema.

“Alikuwa mtu wa starehe na zaidi alipendelea kuvuta sigara, kwenda sehemu za starehe na marafiki zake na alifurahia kuwapa ofa wenzake kama za pombe.”

Mwenyekiti CCM Fire anena

Kuhusu tuhuma kwamba Hamza alikuwa kada wa Chama cha Mapinduzi (CCM), viongozi wa chama hicho tawi la Fire, wameshindwa kuthibitisha hilo baada ya kukosa jina lake kwenye orodha ya wanachama.

Katibu wa CCM Mtaa wa Fire, Hamis Kondo alisema wamepekua nyaraka mbalimbali kujiridhisha kama alikuwa mwanachama wao lakini jina lake halijaonekana.

“Hata sisi tunaona picha mitandaoni akiwa na sare za chama, tukasema ngoja tujiridhishe kama ni mwanachama wetu kwa kuwa ni mkazi wa hapa Fire lakini jina lake halipo.

“Labda alijiunga CCM huko Chunya alikokuwa akifanya shughuli zake lakini kwenye orodha yetu ya wanachama hayupo,” alisema kiongozi huyo wa chama.


Msikiti aliokuwa akiswali

Baadhi ya watu waliokutwa eneo la Masjid Shabhully alipokuwa akiswali Hamza walimwelezea kuwa alikuwa mpole, mwenye upendo na alihudhuria swala.

“Kwa anayemjua hawezi kudhania kuwa ndiye aliyefanya hayo, alikuwa akiswali hapa Magharibi na Isha, mwenyewe alikuwa mpole na mtu aliyependa kujitenga hasa katika siku za hivi karibuni,” alisema mmoja wa watu waliokutwa msikitini hapo.

“Labda akimaliza kuswali kuna muda alikuwa akichezea chezea kompyuta yake.”

Alisema Hamza na familia yake huwa wanaswali katika msikiti huo.

“Alikuwa mtu mzuri sana, lakini hapa katikati alikuwa haonekani, inasemekana alikwenda kusoma, baada ya kurudi mambo yamekuwa mengi, wapo wanaosema hata akili zake haziko sawasawa wakati mwingine lakini kwa kumuangalia yupo sawa, ana upendo kama kawaida,” alidai.

Polisi waliouawa kuagwa leo

Miili ya askari waliofariki dunia inatarajiwa kuagwa leo katika Hospitali ya Polisi Kurasini.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Ramadhani Kingai alisema, “wataagwa kesho (leo) katika Hospitali ya Polisi kule Kurasini, baada ya hapo watasafirishwa kwenda makwao, mmoja ni wa Mbulu, mwingine Katavi na mwingine wa Mwanza,” alisema Kingai kwa ufupi.


Kampuni ya SGA wazungumza

Meneja Uhusiano wa Wateja wa Kampuni ya SGA ambayo askari wake alipoteza maisha katika tukio juzi, Aikande Makere alisema kwa sasa wapo kwenye msiba wa mfanyakazi mwenzao (bila kumtaja jina na kutoa taarifa zake zaidi) na wanasubiri uchunguzi wa polisi ndipo waweze kutoa neno.

“Hili suala ni la polisi zaidi, wao wanafanya uchunguzi hatuwezi kusema chochote, sisi hatukuwepo eneo la tukio tunasubiri watupe ripoti baada ya uchunguzi, hatuwezi kuingilia sasa,” alisema Makere.

Pia, alisema matarajio yao ni kuwa uchunguzi wa polisi utafanyika haraka na majibu yakitoka, kampuni hiyo itaweza kuzungumza lolote.


Taarifa ya Hospitali ya Muhimbili

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Aminiel Aligaesha, walipokea mwili mmoja wa marehemu na majeruhi watano wakiwa na majeraha makubwa na wengine madogo sehemu mbalimbali za miili yao.

Taarifa hiyo inasema kati ya majeruhi hao wanne ni polisi na mmoja ni mlinzi wa kampuni binafsi ya SGA, huku mwili wa marehemu uliopokewa ukiwa ni wa mlinzi wa kampuni hiyo ya ulinzi.

“Baada ya kupokewa, askari wawili (miaka 41 na miaka 49) walikuwa na majeraha makubwa katika sehemu mbalimbali za mwili na viungo vya ndani hivyo kufanyiwa upasuaji wa haraka, upasuaji ulienda vizuri,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo.

“Polisi mwingine mwenye umri wa miaka 35 alipata majeraha mbalimbali makubwa na madogo katika maeneo ya mikono na mgongoni ambaye alipewa huduma stahiki na kufungwa vidonda.

“Askari wa nne (miaka 46), alitibiwa na kuruhusiwa kwa kuwa alikua na majeraha madogo,” inaeleza taarifa hiyo.

“Kwa upande wa mlinzi wa SGA (miaka 42) alikuwa na majeraha ambayo hayakuhitaji upasuaji, hata hivyo alilazwa wodini juzi na aliruhusiwa jana kwenda nyumbani.”

Imeandikwa na Peter Elias, Ephraim Bahemu, Aurea Simtowe, Tatu Mohamed, Temaluge Kasuga na Happiness Samson.