Askofu akutwa amekufa baada ya kutoweka siku tatu

Askofu mstaafu wa Kanisa la Anglikana Tanzania Dayosisi ya Victoria Nyanza (DVN), Boniphace Kwangu
Muktasari:
Askofu mstaafu wa Kanisa la Anglikana Tanzania Dayosisi ya Victoria Nyanza (DVN), Boniphace Kwangu amekutwa amefariki dunia katika mazingira ya kutatanisha.
Mwanza. Askofu mstaafu wa Kanisa la Anglikana Tanzania Dayosisi ya Victoria Nyanza (DVN), Boniphace Kwangu amekutwa amefariki dunia katika mazingira ya kutatanisha.
Marehemu alitoweka tangu Novemba 28 na mwili wake kukutwa ukielea katika Ziwa Victoria eneo la Bukumbi Wilayani Misungwi.
Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu leo Ijumaa Desemba 2, Askofu wa Kanisa la Anglikana Tanzania Dayosisi ya Victoria Nyanza (DVN), Zephania Ntunza amethibitisha kifo cha mtangulizi wake huyo ambaye mwili wake ulikutwa ukiwa umetelekezwa wilayani humo jana.
"Ni kweli Baba Askofu Kwangu ametwaliwa. Bado hatujafahamu kwa kina chanzo cha kifo hiki. Sisi Kanisa na familia tumeliachia Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi kubaini chanzo cha kifo cha mpendwa wetu," amesema Askofu Ntunza.
Akizungumzia taratibu za mazishi, kiongozi huyo wa kiroho amesema; "Tayari tumefanya vikao na familia kuhusu msiba huu mzito lakini bado hatujapanga siku wala eneo la mazishi hadi polisi watakapokamilisha taratibu zao za kiuchubguzi,"amesema.
Kabla ya mwili wake kukutwa Bukumbi wilayani Misungwi, Askofu Kwangu aliyekuwa kiongozi wa nne wa DVN anadaiwa kutoweka kwa siku tatu zilizopita tangu alipoaga familia yake kuwa anaenda wilayani Sengerema kwa shughuli binafsi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa hakupatikana kuzungumzia tukio hilo baada ya kupokea simu yake ya kiganjani na kujibu kuwa yupo kwenye kikao na kuomba atumiwe ujumbe ambao nao haukujibiwa.
Imeandikwa na Saada Amir na Anania Kajuni