ATCL kupunguza safari zake, nyingine kufutwa

Muktasari:
- Mabadiliko hayo yatatokana na changamoto za kiufundi duniani kote ambapo injini aina ya PW1524G-3 zinazotumika kwenye ndege aina ya Airbus A220-300.
Dar es Salaam. Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) limesema litapunguza miruko ya ndege zake sambamba na kufuta baadhi ya safari ili kutoa muda wa matengenezo ya njini.
Mabadiliko hayo yatatokana na changamoto za kiufundi duniani kote ambapo injini aina ya PW1524G-3 zinazotumika kwenye ndege aina ya Airbus A220-300.
Kwa mujibu wa taarifa ya ATCL iliyotolewa leo Alhamisi Novemba 10, 2022, Shirika hilo linaomba radhi kwa usumbufu utakaosababisha na mabadiliko hayo ambayo wanakwenda kuyafanya.
“Kwa kuzingatia matakwa ya usalama, tumekuwa tukifuata maelekezo ya kitaalamu ili kutoa huduma bora nay a usalama. Na wakati mwingine tunazitoa ndege katika mzunguko kukidhi matakwa ya watengenezaji wa injini hizi,” inaeleza taarifa hiyo.
Taarifa hiyo ya ATCL inabainisha kwamba hatua hizo zimesababisha ucheleweshaji wa ndege zao wakati changamoto hiyo ikitafutiwa ufumbuzi.

“Ili kuhakikisha ndege zetu zinafanya kazi kufuatana na ratiba, tutapunguza miruko na kupunguza baadhi ya safari zetu kulingana na idadi ya ndege zilizopo. Uamuzi huu ni wa muda mfupi ili kutoa muda kwa watengenezaji wa injini hizo kushughulikia matatizo yaliyopo,” inaeleza taarifa hiyo.