Aweso awachimba mkwara wakurugenzi mabonde ya maji

Aweso awachimba mkwara wakurugenzi mabonde ya maji

Muktasari:

  • Aweso amesema Wizara ya Maji haiwezi kupiga hatua kama hakuna wasimamizi kwenye mabonde ya maji nchini wanaoshindwa kusimamia majukumu yao katika ushirikishwaji wa wananchi katika utunzaji wa vyanzo vya maji.

Mbeya. Waziri wa Maji, Juma Aweso amesema Wizara yake haiko tayari kufanya kazi na wakurugenzi wa mabonde ya maji nchini wasiotambua majukumu yao na kushindwa kushirikisha wananchi katika utunzaji wa vyanzo vya maji.

Aweso amesema hayo leo Alhamisi Agosti 4, 2022 wakati wa ziara yake ya kufanya uzinduzi wa uwekaji mipaka chanzo cha maji cha Ivumbwe, bonde la Ziwa Rukwa kilichopo kata ya Ivumwe jijini hapa.

“Kama viongozi tuliopewa dhamana na Serikali hatutaweza kukubali wakurugenzi wa maji wanalinda vyanzo vya maji kwenye kompyuta na sasa nataka kusikia wanashirikiana na wadau hususan wa mazingira, TFS kwani kuna mambo ya ajabu yanabainika kwenye maeneo mengi nchini,” amesema.

Amesema kuwa Wizara haiwezi kupiga hatua kama hakuna wasimamizi kwenye mabonde ya maji nchini wanaoshindwa kusimamia majukumu yao katika ushirikishwaji wa wananchi katika utunzaji wa vyanzo vya maji.

“Nasisitiza lazima jamii ishirikishwe katika na Wakurugenzi lazima mkubali kubadilika katika utendaji wa kazi na kwani wananchi wamekuwa mstari wa mbele kutunza na kulinda vyanzo vya maji,” amesema.

Katika hatua nyingine, Aweso ameagiza maeneo yote ambayo wananchi wanatunza vyanzo vya maji wawe mstari wa mbele kupata huduma za maji huku akieleza Serikali imetoa zaidi ya Sh200 bilioni kwa ajili ya miradi mkubwa wa maji mkoa wa Mbeya.

Kwa upande wake, mkurugenzi wa rasirimali ya maji Tanzania, Mhandisi George Lugomela amesema kuwa wana kila sababu ya kuipongeza Wizara ya Maji kwani inaguza maisha ya Watanzania.

Amesema katika kuhakikisha huduma za maji zinaboreshwa wanatarajia kujenga mabwawa makubwa 51 kwa mwaka wa fedha ujao kwa lengo la kuboresha sekta ya mifugo na kilimo sambamba na kulinda hifadhi ya mita 60 kutoka vyanzo vya maji.

Ofisa bonde la Maji ziwa Rukwa, Grace Chitanda amesema kuna vyanzo vya maji 36 vimewekwa mipaka na 24 vipo katika maeneo lindwa kwenye mpaka namba GN 236.

Akizungumza kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Mbeya, mkuu wa wilaya ya Mbeya, Dk, Rashid Chuachua amesema wako nyuma ya Wizara ya Maji katika kuhakikisha vyanzo vya maji vinalidwa ili jamii iweze kupata maji safi na salama.

Mkazi wa Ivumwe, Jane Solomon amesema uamuzi wa Wizara ya maji kuweka mikakati kwenye hifadhi za vyanzo vya maji utasaidia kudhibiti shughuli za kijamii kwenye vyanzo na usalama wa maji.